Mbowe ataja siri ya mshikamano Chadema

Muktasari:

      Asema wanafanya kazi kama watu wa familia moja

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema siri ya mshikamano wa viongozi wa chama hicho inatokana na kufanya kazi kama watu wa familia moja bila ya kujali nafasi zao za uongozi.

Mbowe alisema hayo juzi mara baada ya ibada ya mazishi ya Anastazia Mayunga ambaye ni mama mzazi wa wakili maarufu wa kujitegemea Peter Kibatala katika Kanisa la Mtakatifu Maria Consolata Parokia ya Sua.

Alisema Chadema imeguswa na msiba wa mama wa wakili huyo ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa akiwatetea viongozi wa chama hicho na wanachama wake katika kesi mbalimbali zinazowakabili.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa wakili Kibatala Chadema imeamua kuahirisha kikao cha Kamati Kuu ambacho kilipaswa kuketi leo ili kutoa fursa kwa viongozi wake wakuu kuhudhuria mazishi ya mama yake mzazi ambaye alifariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi.

Katika salamu zake rambirambi, mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Suzan Kiwanga alisema msiba wa mama wa wakili Kibatala umewagusa wanachama na viongozi wengi wa chama hicho hasa wale ambao walishawahi kuwa na kesi mbalimbali ambazo wakili huyo aliwatetea.

“Mara nyingi kwenye hizi kesi tunazofunguliwa mahakamani... Kibatala amekuwa akitumia muda na uzoefu wake wa kisheria kuhakikisha tunashinda, mimi kwangu namfananisha na mwanangu na kwenye maisha yake naahidi kuchukua nafasi kama mama yake,” alisema Kiwanga.

Omary Kondo ambaye ni mwenyekiti wa Mtaa wa Fockland ambao marehemu alikuwa akiishi, alisema mama huyo alipoteza maisha kutokana na kuangukiwa na kifusi kilichotokana na mvua ambazo pia zimesababisha nyumba tano kubomoka katika mtaa wake.

Akisimulia chanzo cha kifo hicho kilichotokea Alhamisi iliyopita, Kondo alisema baada ya mvua kubwa kunyesha mama Kibatala aliyekuwa akiishi katika Kata ya Mlimani alimwita kijana wake wa nyumbani ili amsaidie kuchimba mfereji wa kupitisha maji.

Alisema wakati kijana huyo alipoenda kuazima jembe ndipo kifusi kilipoporomoka ghafla kutoka mlimani na kumfukia.

“Baada ya yule kijana kurudi akiwa na jembe alikuta kifusi kimemfunika mama Kibatala, sehemu ya kichwani tu ndiyo iliyokuwa ikionekana. Pamoja na jitihada za wananchi kufukua kifusi hicho, baadaye ilibainika kuwa mama Kibatala alishafariki dunia,” alisema Kondo. Mama Kibatala alizaliwa Juni 16, 1957 mkoani Shinyanga na aliwahi kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma na Jimbo Katoliki Arusha.