Mbowe atupiwa virago nje

Mkurugenzi wa Nhc , Nehemiah Mcheche

Muktasari:

Agosti 24, Mkurugenzi wa NHC, Nehemiah Mchechu alisema wadaiwa sugu akiwamo Mbowe wataondolewa kwenye majengo ya shirika hilo iwapo watashindwa kulipa madeni wanayodaiwa baada ya kupewa notisi ya mwezi mmoja.

Dar es Salaam. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limeanza mchakato wa kuwanyang’anya mali na kuwaondoa kwa nguvu wadaiwa sugu kwenye majengo yake wakianza na mmiliki wa jengo la Club Bilicanas, Freeman Mbowe.

Agosti 24, Mkurugenzi wa NHC, Nehemiah Mchechu alisema wadaiwa sugu akiwamo Mbowe wataondolewa kwenye majengo ya shirika hilo iwapo watashindwa kulipa madeni wanayodaiwa baada ya kupewa notisi ya mwezi mmoja.

Inadaiwa kuwa Mbowe kupitia kampuni yake ya Mbowe Hotels Limited (MHL), ilikodi jengo la NHC alilokuwa  akilitumia kwa biashara  ambalo linadaiwa kuwa na limbikizo la deni la Sh1.2 bilioni.

Jana kuanzia saa 1.30 asubuhi, NHC chini ya madalali wake iliwasili eneo lilipo jengo hilo ili kutekeleza uamuzi huo wa kumuondoa mmiliki huyo kwa kutoa nje vitu vilivyokuwa ndani ya ofisi za Free Media ambayo huchapisha gazeti la Tanzania Daima.