Mbowe awalipua madiwani Chadema waliohamia CCM

Aliyekuwa Diwani wa Chadema Kata ya Kaloleni jijini Arusha, Emmanuel Kessy akifurahia baada ya kujiuzulu na kujiunga CCM. Picha na Mussa Juma

Dar es Salaam. Wakati madiwani wa Chadema wakiendelea kuhamia CCM, viongozi wakuu wawili wa chama hicho wametoa sababu za wanasiasa hao kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema madiwani hao wanahama kwa sababu walitarajia kupata masilahi binafsi ambayo wameyakosa.

“Waliojiunga na Chadema kufuata masilahi wamekuta hakuna, hapa ni wito, ndiyo hao wameondoka,” alisema.

Wakati Mbowe akisema hayo, katibu mkuu wake, Vincent Mashinji amedai makada hao wanahama kwa ahadi ya kulipiwa mikopo wanayodaiwa kwenye taasisi za fedha.

“Baadhi ya madiwani walikuwa wanadaiwa mikopo na taasisi za fedha, sasa wamelipiwa baada ya kununuliwa,” alisema.

Kauli za viongozi hao zimekuja siku moja baada ya diwani wa Chadema, Kata ya Kaloleni mkoa ni Arusha, Emmanuel Kessy kujiuzulu juzi saa sita usiku na kujiunga na CCM huku akitoa sababu tatu za uamuzi huo.

Kessy ambaye anakuwa diwani wa 22 kuhama chama hicho mkoani Arusha alitaja sababu hizo kuwa ni kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kazi yake kupambana na rushwa, ufisadi na kuwaletea maendeleo wananchi.

Sababu ya pili alisema ni kupunguza msuguano uliopo baina yake na viongozi wa Chadema na tatu alidai anaamini akiwa CCM atarahisisha utendaji kazi wake.

Kessy alisema alichukua uamuzi wa kujiuzulu saa 6:30 usiku baada ya majadiliano na viongozi wa CCM waliokuwa wakimshauri.

“Kujiuzulu usiku ilitokana na kufikia makubaliano tu kwani siku nyingi nilikuwa nikiombwa na watu mbalimbali na huu ni uamuzi wangu,” alisema.

Alisema CCM ikimuona anafaa na ikampitisha kugombea tena udiwani, ataendeleza mipango yote ya maendeleo ambayo alikuwa anaifanya.

Kuhusu madai ya kununuliwa, alikanusha akisema aliamua kuhamia CCM kumuunga mkono Rais Magufuli.

Mtazamo wa Mbowe

Akizungumza jana, Mbowe alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Chadema ilipata madiwani 1,184 lakini hadi sasa waliojiuzulu ni kati ya 30 hadi 40.

“Ingawa hatufurahii madiwani kujiuzulu, lakini siyo tishio kwa chama kwani sababu wanazozitoa hazina maana,” alisema.

Kuhusu madai ya madiwani wanaohama kwamba ni kuunga mkono utendaji kazi wa Rais Magufuli alisema, “Wanaunga mkono wakati ajira zimepotea, hakuna demokrasia, biashara zimefungwa.”

Mbowe alisema madiwani wanaounga mkono juhudi za Rais Magufuli hawafai kuwapo Chadema kwa sababu si wa kweli.

“Hatuwahitaji madiwani wanaounga mkono utendaji wa Serikali wakati kuna changamoto nyingi, kama bado wapo wa aina hiyo bora waondoke,” alisema.

Mbowe alisema suala la madiwani kuhama Chadema ni la mpito na haliwezi kuwa la kudumu.

“Hizi ni siasa chafu haziwezi kuwa za kudumu zitapita, lakini kikubwa kwamba tuko imara tunaendelea kukijenga chama,” alisema.

Katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, Mashinji alisema hatua ya madiwani hao kujiuzulu ni haki yao.

“Hiki ni chama cha demokrasia na maendeleo, diwani kuhama ni haki yake lakini siyo tishio kwa chama,” alisema.

Alisema makada wa chama hicho waliopikwa na kuiva bado wanaendelea kuwa wanachama waaminifu.

“Hakuna tishio kabisa kwa chama madiwani hao kuhama. Jambo lenyewe linakuzwa ili ieleweke kwamba Chadema inakufa, lakini hali haiko hivyo,” alisema Mashinji.

Wasomi wazungumza

Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki Iringa (Rucu), Gaudence Mpangala alisema viongozi wa Afrika, Tanzania ikiwamo, wanaviona vyama vya upinzani kama maadui na siyo wadau wa maendeleo kwenye nchi zao, “Huu mchezo wanaoufanya madiwani wa Chadema kuhamia CCM huhitaji kufikiria sana ili kufahamu kinachoendelea.”

Profesa Mpangala alisema viongozi wa aina hiyo ni wa kuogopwa kwa sababu hata huko walikohamia wanaweza kuhama tena.

“Kiongozi umechaguliwa na wananchi ambao wamekuamini kabla ya kumaliza muda unajiuzulu kwa sababu rahisi,” alisema.

Madiwani waliohama Arusha

Hadi juzi usiku, madiwani wa Chadema katika Mkoa wa Arusha waliohamia CCM walifikia 22 wa mwisho akiwa Kessy.

Februari 15, madiwani watatu walijiuzulu kwa pamoja katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Madiwani hao na kata zao kwenye mabano ni Daniel Olkery (Ngorongoro), Lazaro Saitoti (Ngoile) na Sokoine Moir (Alaitole).

Ngome ya Chadema Iringa

Katika Mkoa wa Iringa pekee, madiwani sita wa Chadema walikuwa wamejiuzulu hadi kufikia Januari na kujiunga na CCM.

Madiwani hao na majina yao kwenye mabano ni Tundesy Sanga (Ruaha), Joseph Ryata (Kwakilosa), Baraka Kimata (Kitwiru), Edger Mgimwa (Kilosa), Leah Mlele (Viti Maalumu) na Husna Daudi (Viti Maalumu).