Mbunge: Tatizo la uchaguzi ni usaliti

Muktasari:

  • Ataja mambo mengine matatu, katibu UVCCM Mbeya adai wao ulikuwa shwari

Uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), umeendelea kuwapasua vichwa makada wake, safari hii mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Mbeya, Dk Mary Mwanjelwa akiainisha mambo kibao yanayowatesa, ikiwamo usaliti.

Juzi,kada mwingine wa CCM kutoka mkoani Morogoro, Mariam Kambi alilalamikia matumizi ya rushwa kumwangusha katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT).

Katika kinyang’anyiro hicho, Kambi aliangushwa na Lidya Mbeaji aliyedai kwamba ushindi wake ulikuwa na msukumo wa fedha akimtuhumu mmoja wa wabunge kufanikisha jambo hilo.

Hata hivyo, mgombea huyo aliahidi kukata rufaa katika vikao husika ndani ya chama chao.

Akizungumzia uchaguzi ndani ya chama hicho, Dk Mwanjelwa alisema siasa ndani ya chama ni ngumu na zinaumiza kichwa kila wakati hususan unapofika wakati wa uchaguzi.

Dk Mwanjelwa ambaye amekuwa akirudiarudia kauli hiyo tangu kuanza kwa chaguzi ndogo ndani ya chama hicho na juzi kwenye uchaguzi wa UWT Mbeya mjini alikuwa mgeni rasmi na hakusita kusema ugumu wa siasa unatokana na kusalitiana. “Siasa za Mbeya mjini ni ngumu sana na zinaniumiza kichwa kwani wanachama ndani ya chama chetu tumekuwa si watu wa kuaminiana kwani wamejaa usaliti, unafiki, tamaa ya fedha na ukabila,” alisema mbunge huyo.

Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mbeya Mjini, Gerald Kinawiro alisema mchakato wa kuwapata wagombea katika nafasi mbalimbali ndani ya umoja huo ulizingatia vigezo vyote kulingana na kanuni za chama chao.

“Uchaguzi wa mwaka 2017 umefanyika kwa haki na uwazi kwani hakuna kiongozi yeyote aliyepitishwa kwa kuangalia urafiki wa karibu au uwezo wa kifedha, wote wamepitishwa kwa kuangalia vigezo ambavyo vipo kwenye katiba ya CCM,” alisema Kinawiro.

Mwenyekiti wa CCM Mbeya Mjini, Ephraim Mwaitenda aliwataka viongozi wanaochaguliwa katika chaguzi hizo kutambua dhamana kubwa ya kukijenga chama hicho.

“Msiwe chanzo cha kuleta makundi ndani ya umoja huo, kwani makundi hayo yalisumbua sana kwenye chaguzi na hata utendaji wa shughuli za kichama,” alisema.