Mgaya amwaga vyerehani vya kufungua viwanda 92 Njombe

Muktasari:

Mbunge huyo ametoa vyerehani hivyo 370 ambavyo ukivigawa kwa vinne vinne ambavyo utapata viwanda 92.

Njombe. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Mgaya ametoa msaada wa vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Sh 90 milioni kwa wanawake mkoani humo ili wajikwamue kiuchumi huku akiunga mkono juhudi za Serikali inayohimiza uchumi wa viwanda.

Akizungumza mjini Makambako wakati wa hafla ya kukabidhi vyerehani hivyo kwa baadhi ya wanawake, Mgaya amesema amefikia uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa Taifa la uchumi wa kati kupitia viwanda.

Ameeleza juhudi za kumkomboa mwanamke wa Mkoa wa Njombe ni jambo linalopiganiwa kwa miaka mingi hivyo vyerehani hivyo vitawafungulia njia kuweza kujikwamua kiuchumi.

“Nimekuwa sina papara katika utendaji wangu, mwaka jana nilitoa msaada wa vitabu vya ziada kwa Shule za Sekondari Halmashauri ya Makambako, ambapo kwa mwaka huu nimeamua kuunga mkono juhudi za Serikali upande wa viwanda kwa kuwasadia wanawake hawa vyerehani hivi 370,” alisema Mgaya.

Akifafanua amesema anatambua thamani kubwa walionayo wanawake hivyo kwa kuwawezesha vyerehani hivyo kutainua familia na jamii zinazowazunguka kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia huduma za kijamii na mahitaji mengine.

“Mtu ninayemthamini huwa nampa kitu ambacho kitadumu na kumsaidia kwa muda mrefu, mimi nimeamua kutowapa samaki kwani mtamla ataisha, nimewapa nyavu ambayo mtaitumia kuvua samaki, nendeni mkavitunze vyerehani hivi kujiletea maendeleo endelevu,” alisema Mgaya.

Akizungumza baada ya kupokea cherehani yake Diwani wa Viti Maalum Lupembe, Neema Limbanga amesema alilolifanya mbunge huyo wa Viti Maalum halijawahi kutokea katika maisha yake na kwamba vyerehani hivyo vimewafungulia njia kimaisha.