Mbunge CCM, mwenyekiti wake wahojiwa polisi kwa amri ya DC

Muktasari:

  • Akizungumza leo Alhamisi Machi 8, 2018 Msafiri amekiri kuagiza viongozi hao kukamatwa na polisi jana kwa maelezo kuwa waliendelea kufanya mikutano iliyopigwa marufuku.

Hanang. Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu na mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa, Mathew Darema wamehojiwa kituo cha polisi Katesh kwa amri ya mkuu wa wilaya hiyo, Sarah Msafiri  wakidaiwa kuichonganisha Serikali na wananchi. 

Akizungumza leo Alhamisi Machi 8, 2018 Msafiri amekiri kuagiza viongozi hao kukamatwa na polisi jana kwa maelezo kuwa waliendelea kufanya mikutano iliyopigwa marufuku.

Msafiri amedai Nagu amekuwa akiwaambia wananchi kuwa ziara za mkuu wa wilaya hazina tija na wazikatae kwani yeye kama mbunge amezipiga marufuku. 

Msafiri amesema pia mbunge huyo amekuwa akiwaambia wananchi kuwa Sh300 milioni za halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa wanawake na vijana hazijulikani zilipo wakati akitambua kuwa suala hilo ni la mwaka 2014 na limeshapatiwa ufumbuzi.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa ilani ya CCM unaenda vizuri na uhusiano kati ya Serikali na chama hicho tawala uko vizuri.

"Mwenyekiti wa CCM ndiye katibu wa mbunge, kuna muda anatekeleza ukatibu wake lakini bado anaendelea na uenyekiti wake, ila hakuna anayeonewa na tukumbushane kufuata sheria," amesema Msafiri. 

Amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imefanya mambo mengi Hanang' ikiwemo kutoa Sh60 milioni za mikopo kwa vikundi, kutoa eka 400 za kilimo na kuwatafutia ajira za kudumu vijana 270 waliomaliza mgambo. 

"Kiongozi yeyote anapofanya makosa ambayo hakutumwa na mamlaka yoyote au chama chake basi awajibike mwenyewe tusitumie taasisi kama kichaka cha kujificha," amesema Msafiri. 

Hata hivyo, Dk Nagu alipotafutwa na MCL Digital kutoa ufafanuni kuhusu suala hilo amesema, “wewe zungumza na mkuu wa wilaya juu ya hilo lakini kwa upande wangu sitaki kuongelea chochote kuhusu hilo uliloniuliza.”

Naye Darema amesema mbunge ana haki ya kikatiba kufanya mikutano, lakini mkuu huyo wa wilaya anakumbatia na kuficha maovu yaliyopo eneo hilo. 

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Agostino Senga amethibitisha kushikiliwa polisi na kuhojiwa kwa Dk Nagu na Darema. 

"Walihojiwa polisi kwa amri ya mkuu wa wilaya ila hawakulala tuliwaachia na kuwaagiza warudi leo asubuhi kwa ajili ya kuendelea na mahojiano hayo," amesema.