Mbunge CUF adai Serikali ‘inabeti’, azua hekaheka bungeni

Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmadi Katani akizungumza alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Kauli hiyo aliyoitoa leo Mei 15, 2015 katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19 ulimuinua kwenye kiti  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na kusema kauli ya Katani inawadhalilisha walioko serikalini.

 Dodoma. Kauli ya  mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani ya kufananisha utendaji kazi wa Wizara ya Kilimo na michezo ya kubahatisha maarufu kama ‘kubeti’ imezua kisaazaa bungeni.

Kauli hiyo aliyoitoa leo Mei 15, 2015 katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19 ulimuinua kwenye kiti  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na kusema kauli ya Katani inawadhalilisha walioko serikalini.

Katika maelezo yake Katani amesema hadi leo mawakala wanaosambaza pembejeo hawajalipwa fedha zao.

Amesema Sh200bilioni  zilizotakiwa kwenda katika mfuko wa korosho hazijaenda kwa miaka yote kwa ajili ya kukuza zao.

 

“Serikali hii imekuwa ya kubeti beti na kwenye  kilimo imekuwa ikibeti. Fedha za korosho za export levy (ushuru wa mazao yanaouzwa nje) Sh206bilioni hazilipi. Mnacheza na  kilimo, mnawadanganya wakulima wa korosho,”amesema.

Amesema Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amekuwa akikibeba chama cha ushirika cha Tanecu kwa kukiombea kukopeshwa fedha Sh 200bilioni.

Amehoji pia sababu ya msingi ya kumuondoa mkurugenzi wa bodi ya korosho na kuwaacha watendaji.

“Kwanini wasingeondolewa watendaji? Hakuna maelezo yanayotosheleza yaliyosababisha mkurugenzi huyu kuondolewa,”amesema.

Hata hivyo, Katani aliombewa utaratibu na Mhagama kuwa lugha anayoitumia inadhalilisha watu wanaofanya kazi Serikalini kwasababu neno kubeti lina maana ya kubahatisha.

Hatua hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge kumtaka kufuta maneno hayo lakini Katani akaendelea kufafanua alichokuwa akikikimaanisha na hivyo kutakiwa na kiti kutoendelea kuchangia.