Mbunge CUF amwaga chozi, ampiga ‘stop’ Dk Mpango kukanyaga Lindi na Mtwara

Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmadi Katani akiengua kilio baada ya kumaliza kuchangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Mbunge wa Tandahimba (CUF), Ahmad Katani amemwaga chozi bungeni na kumshukia  Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwamba kama Serikali haitatoa asilimia 65 ya fedha za ushuru wa mauzo ya korosho nje, asikanyage mikoa ya Lindi na Mtwara.

Katani ametoa kauli hiyo leo jioni Juni 25, 2018 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2018/19.

Mbunge huyo amezungumza kwa dakika tano na katika muda wote aliokuwa akizungumza alikuwa akibugujikwa na machozi.

“Fedha za korosho zipo kisheria na wale wanaochangia kinyume cha hapo wakisema ni za mfuko mkuu wanapotosha Watanzania kuonyesha watu wa kusini wanazitaka kwa maendeleo ya kusini,” amesema.

Huku akisisitiza kuwa Korosho inalimwa zaidi Mtwara na Lindi amesema, “hizi fedha tusipozipata Dk Mpango usikanyange Lindi na Mtwara. Hata fedha zilizopo kisheria unazichukua?”

“Wewe (Dk Mpango) ni waziri wa ajabu ambaye hujapata kutokea. CCM mnasema ni chama cha wanyonge, wanyonge hao wa aina gani? Wakulima wanaolima korosho kwa jembe la mkono mnachukua fedha zao huna huruma. Mnapotosha umma wa watanzania,  mmekuja bungeni kusimamia watanzania lakini mnashangilia wanavyoonewa na kudhurumiwa. Hawa wabunge wanaotoka majimbo ya Ikulu ni shida sana.”