Mbunge Chadema aachiwa kwa dhamana

Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka.

Muktasari:

Ni Frank Mwakajoka wa Tunduma alikamatwa jana baada ya kwenda kituo cha polisi kuomba ulinzi wa askari

Tunduma. Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka na katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) Mkoa wa Songwe, Ayub Sikagonamo wameachiwa kwa dhamana leo jioni Jumapili Julai 15, 2018.

Viongozi hao walikamatwa na polisi jana baada ya kwenda kituo cha polisi kuonana na mkuu wa kituo hicho (OCD) ili awape ulinzi wa askari.

Walichukua uamuzi huo ili kwenda na askari hao katika ofisi za Halmashauri ya Tunduma kuchukua fomu za wagombea udiwani wa chama hicho. Awali walikwenda katika ofisi hizo na kukuta zimezingirwa na polisi.

Akizungumza baada ya kuachiwa huru, Mwakajoka amesema wakiongozwa na wakili wao Boniphace Mwabukusi, wameelezwa kuwa wanatuhumiwa kwa kosa la kuchoma moto nyumba ya mgombea wa udiwani kata ya Mwaka Kati, Ayub Mlimba (CCM).

“Ni mambo ya ajabu sana. Sisi  tulikwenda Polisi kuomba ulinzi ili tusindikizwe katika ofisi za halmashauri kuchukia fomu za wagombea wetu. Eneo lile kulikuwa na ulinzi na tulijua tukienda tunaweza kuambiwa  tumekwenda kufanya vurugu,” amesema Mwakajoka.

“Tulikataliwa na wakati tukijiuliza sababu tukaelezwa kuwa tupo chini ya ulinzi, kutuhumiwa kuwa tumechoma moto nyumba ya mgombea wa CCM.”

Wakati Mwakajoka na Sikagonamo wakiachiwa wa dhamana, wanachama 15 wa Chadema wameendelea kusota mahabusu baada ya kukosa dhamana.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, wanachama hao wanatuhumiwa kufanya shambulio kali licha ya shambulio husika kutowekwa wazi.