Mbunge Chadema aibua sakata la uchaguzi kata 43

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kikao cha nane cha mkutano wa kumi wa Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Alisema badala yake, wagombea wa CCM ndio waliotangazwa kuibuka na ushindi, huku akizitaja baadhi ya kata ambazo alidai kuwa Chadema ilishinda.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Devotha Minja jana aliibua bungeni sakata la uchaguzi wa udiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba mwaka jana akidai kwamba baadhi ya wagombea wa Chadema walishinda, lakini hawakutangazwa kuwa washindi.

Alisema badala yake, wagombea wa CCM ndio waliotangazwa kuibuka na ushindi, huku akizitaja baadhi ya kata ambazo alidai kuwa Chadema ilishinda.

Devotha alisema hayo katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alijibu kuwa hajui kama kuna kata ambayo mgombea wa Chadema alishinda na hakutangazwa.

Alisema utangazaji wa matokeo una taratibu zake ambazo huvishirikisha vyama husika vilivyosimamisha wagombea.

Katika swali lake, Devotha alisema anao ushahidi kuwa katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata 43 uliofanyika Novemba 26 mwaka jana, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kiliporwa ushindi huku wagombea wa CCM, wakitangazwa kuibuka kidedea.

Matokeo rasmi yanaonyesha kuwa katika uchaguzi huo, Chadema ilishinda kata moja, huku CCM ikiibuka na ushindi katika kata 42.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni tulikuwa na chaguzi ndogo katika majimbo na kata 43 nchini kote, lakini uchaguzi huo uligubikwa na hila na manyanyaso kwa kutowatangaza wagombea walioshinda, badala yake ushindi wakapewa watu wengine. Je, Serikali inasema nini juu ya jambo hilo?” aliuliza Devotha.

Mbunge alisema katika Kata ya Sofi, Mkoa wa Morogoro, mgombea wa Chadema alipata kura 1,908 wa CCM 1,878 na Kata ya Siyui mkoani Singida, Chadema ilipata kura 1,358 na CCM 1,304 lakini washindi waliotangazwa ni wagombea wa CCM.

Katika majibu yake, Waziri Mkuu alisema hajui kama kuna kata ambayo Chadema ilishinda na haikutangazwa.

Pia alisema hadhani kama Tume inaweza kuwatangaza walioshindwa na kuwaacha washindi kwa maelezo kuwa kila kitu kinafanyika chini ya ushirikishwaji wa vyama husika vilivyoweka wagombea kwenye maeneo husika.

“Lakini sheria zinaipa nafasi Tume ya Taifa ya Uchaguzi nafasi ya kukutana na vyama vinavyogombea ili kuwepo na nafasi ya kujadiliana kwenye mapungufu,” alisema.

Alisema sheria zimeipa mamlaka NEC kukutana na kujadiliana na vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea na kwamba Katiba imetoa nafasi pia ya kukata rufaa mahakamani.

Hivyo, Waziri Mkuu aliwataka wanaohisi kuonewa waende mahakamani kudai ushindi wao katika kipindi kisichozidi miezi mitatu ili sheria itazamwe kwenye ushindi huo.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Chadema ilieleza changamoto kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi huo, ikiwamo ya mawakala wake kuzuiwa katika vituo vya kupigia kura na kuiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuyafanyia kazi.

Kutokana na madai hayo, Desemba 17 mwaka jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutano uliovihusisha vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chaumma ambacho kilialikwa, alitangaza kutoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Januari 13 huko Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido.

Alisema vyama, NEC na Serikali vilipaswa kukaa katika meza ya majadiliano, kusitisha uchaguzi wa ubunge wa Januari 13 ili wadau wakutane kufanya tathmini ya changamoto zilizojitokeza.

Katika swali jingine, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali inapambana kufufua mazao makuu matano ambayo yalikuwa yameshuka uzalishaji wake lakini pia kutafuta masoko kwa uhalisia. Aliyataja mazao hayo kuwa ni pamba, chai, korosho, tumbaku, kahawa na pamba.

Alikuwa akijibu swali la Richard Ndasa (Sumve) na Zuberi Kuchauka (Liwale).

Kuhusu pamba, alisema mkakati ni kulihuisha zao hilo na kulifanya lirudie katika hadhi yake iliyokuwa imepotea baada ya wakulima kuanza kukata tamaa kutokana na kukosa masoko na usimamizi wakutosha.

Hata hivyo, alisema kati ya Februari 15 na 17 atakwenda mkoani Mwanza kwa lengo la kukutana na wafanyabiashata wote wanaohusiana na zao hilo ili kuzungumza nao na kuona namna bora ya kuliongezea thamani.

Akizungumzia korosho alisema zao hilo kama ilivyo kwa mengine, lilishapoteza mwelekeo kwa miaka mingi na kuwa hali ikiachwa inaweza kuwa mbaya zaidi na kulipoteza.

Aliwashauri wakulima wa zao hilo kuwa makini zaidi kwa kutunza fedha za mauzo kwa lengo la kununua mbolea na vifaa vingine kwani mwaka jana walipewa mbolea lakini kwa msimu huu watatakiwa kujinunulia.