Thursday, June 14, 2018

Mbunge Chadema aipongeza serikali kufuta kodi taulo za kike

 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi Iyamola@mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza ameipongeza Serikali kwa kufuta kodi ya taulo za kike.

Soma bajeti nzima hapa: http://bit.ly/BAJETIMW

Peneza amesema hatua hiyo itawawezesha wanafunzi waliokuwa wanashindwa kupata taulo hizo kuzipata na kuhudhuria masomo kama kawaida.

Kufutwa kwa kodi hiyo kumetangazwa bungeni leo Juni 14,2018 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akisoma Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19.

Februari mwaka huu, bunge lilikataa hoja binafsi ya Peneza  kuhusu kugawa bure taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi nchini.

Akizungumza na Mwananchi, Peneza amesema,anaishukuru  Serikali kwa kufuta kodi hiyo kwani ni ishara kwamba Serikali imesikia maoni ya wadau mbalimbali.

Peneza amesema kinachopaswa kufanywa sasa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujipanga kufuatilia ili kuhakikisha pedi zinapatikana kwa gharama nafuu.

"Kwa kuwa kodi imefutwa, matarajio yangu ni kwamba, idadi ya watumiaji wa pedi itaongezeka, kwa hiyo niombe TRA ijipange ili zipatikane kwa bei ya chini na kwa wingi," amesema Peneza

Soma bajeti nzima hapa: http://bit.ly/BAJETIMW


-->