Mbunge Chadema aisukumia mzigo CCM

Muktasari:

Amesema asilimia 75 wa Watanzania wanategemea kilimo, lakini Serikali imeshindwa kuwasaidia na kukimbilia kununua ndege.


Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Paresso amesema wakulima wanatakiwa kutambua kuwa adui yao namba moja ni chama tawala, CCM akisema

haiwezekani asilimia 75 ya Watanzania wanaotegemea kilimo, lakini imeshindwa kuwasaidia.

Amesema  Serikali imeshindwa kuwekeza fedha za kutosha katika kilimo huku kwa upande wa asilimia tano ya Watanzania wanaotumia usafiri wa anga ndege zimenunuliwa.

Paresso ametoa kauli hiyo leo Mei 15, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2018/19 ambapo wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh170.2bilioni.

Amesema  kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonyesha ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2011 ilikuwa asilimia 1.9, mwaka 2012 (3.2), mwaka 2013 (4), mwaka 2014 (3.4), mwaka 2015 (3.2), mwaka 2016 (1.9) na mwaka 2017 kwa asilimia 1.3.

“Sekta hii kama itawekeza vizuri itatoa ajira, kuondoa umasikini na tutafikia hicho mnachosema uchumi wa viwanda, lakini sekta hii imekuwa haipewi fedha kama inavyotakiwa na fedha tunazozitenga hazifiki,” amesema Paresso.

“Serikali ya Awamu ya Nne inaondoka madarakani iliacha kilimo kinakua kwa asilimia 3.2, ila hii Serikali ya Awamu ya Tano inayojiita uchumi wa viwanda, kimeendelea kushuka na kufikia asilimia1.9.”

Amesisitiza, “wakulima wa nchi hii wanapaswa kujua adui yao ni Serikali, asilimia 75 wanategema kilimo lakini asilimia tano ya Watanzania wanaotegemea usafiri wa anga wanawepa ndege. Huku ni kuwahadaa wakulima ambao wanapaswa kujua Serikali ya CCM ndio adui yao.”