VIDEO: Mbunge Chadema apinga idadi ya abiria waliokuwa kwenye kivuko

Muktasari:

  • Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi amesema kivuko cha MV Nyerere kilibeba abiria zaidi ya 300

Ukerewe. Wakati Serikali ikisema miili 224 imeopolewa baada ya kivuko cha MV Nyerere kuzama, mbunge wa Ukerewe (Chadema) Joseph Mukundi amedai idadi ya abiria waliokuwa kwenye kivuko hicho ni zaidi ya 300.

Kivuko hicho kilizama Septemba 20, 2018 mita 50 kabla ya kutia nanga kwenye gati la Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe.

Mkundi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 23, 2018, saa chache baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kusema kuwa kivuko hicho kilikuwa kimepakia abiria 265 wakati kina uwezo wa kubeba watu 101.

 

Akitoa mchanganuo wa vifo, Waziri Kamwelwe amesema wanawake 126, wanaume 71, watoto wa kike 17, watoto wa kiume 10 na kufanya jumla ya maiti 224.

Akizungumza na MCL Digital leo mbunge huyo amesema kulingana na mazingira na changamoto za usafiri kati ya Bugolora na Ukara, ni wazi kuwa abiria katika kivuko hicho walikuwa zaidi ya 300.

"Hili suala niliwahi kuliwasilisha bungeni lakini kilichofanyika ni ununuzi tu wa injini mpya," amesema Mkundi.

“Serikali ina majukumu mawili, la kwanza ni kununua kivuko kikubwa na pili ni kuongeza safari za kivuko kutoka safari mbili kwa siku hadi nne ili kuzuia upakiaji wa abiria kupita kiasi.”

Mkundi amesema Ukara ni kata kubwa ambayo inahitaji siku maalum ya gulio, si wananchi wake kwenda Bugolora kila wakati kwa ajili ya kununua bidhaa.

Mbunge huyo ameungwa mkono na mwenyekiti wa kijiji cha Bwisya, Oru Magero aliyesema kuwa ni kawaida kushuhudia kivuko cha Mv Nyerere kikiwa kimepakia mizigo na abiria kupita kiasi.

"Serikali isaidie wananchi wa Ukara kuwaboreshea usafiri kama sehemu nyingine za  nchi yetu," amesemaMagero.