Mbunge Chadema ataka serikali ichukue uwanja wa ndege Tarime

Muktasari:

Kwa sasa umekodishwa kwa mwekezaji wa kampuni ya Coastal Aviation kwa mkataba  wa kulipa Sh20 milioni kila mwaka

Dodoma. Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema) ameitaka Serikali kuuchukua uwanja wa ndege Tarime ambao umekodishwa kwa mwekezaji.

Matiko ameliambia Bunge leo kuwa uwanja huo una manufaa makubwa kwani unaweza kupokea hata ndege za kutoka nje huku mwekezaji akikusanya mapato mengi zaidi.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kandege alisema kiwanja hicho cha Magena ni kinamilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Tarime na kina urefu wa mita 1,470 na upana wa mita 120.

Alisema kwa sasa kiwanja hicho kimekodishwa kwa mwekezaji kampuni ya Coastal Aviation kwa mkataba wa kulipa Sh20 milioni kila mwaka.

Alisema Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Tarime ina mpango wa kujenga ofisi za uhamiaji ili kuweka utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka kwa watalii wanaokwenda hifadhi ya taifa ya Serengeti kupitia kiwanja hicho.