Mbunge Hafsa Mosi auawa Burundi

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki nchini Burundi Hafsa Mossi ameuawa na watu wasiojulikana mjini Bujumbura

Muktasari:

  • Mauaji hayo yameongeza hali ya wasiwasi huku pia mazungumzo ya amani yanayofanyika Arusha yakiripotiwa kukwama..

Kigali, Burundi. Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki nchini Burundi Hafsa Mossi ameuawa na watu wasiojulikana mjini Bujumbura.

Mauaji hayo yameongeza hali ya wasiwasi huku pia mazungumzo ya amani yanayofanyika Arusha yakiripotiwa kukwama.

Mossi, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika Serikali ya nchi hiyo, aliuawa kwa kupigwa risasi katika barabara ya Gihosha, eneo la Nyankoni.

Mbunge huyo aliwahi kufanya kazi na idhaa ya Kiswahili ya BBC kabla ya kurejea nyumbani na kuwa msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza. Baadaye alijiingiza rasmi katika siasa.

Msemaji wa Rais wa Burundi Willy Nyamitwe amesema kuwa mauaji hayo yameleta pigo kubwa kwa wananchi wa Burundi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Alain Aime Nyamitwe ametoa taarifa akielezea masikitiko yake kuhusiana na mauaji hayo.