Mbunge Mattembe amwaga mifuko ya saruji Singida

Muktasari:

Asema dhamira ni kuona jamii ya Watanzania inabadilika na kuwa bora zaidi


Singida. Watanzania wametakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu na afya ili kuendelea kujenga Taifa bora.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, amesema hayo jana, Machi 23, 2018 wakati akikabidhi msaada wa mifuko 600 ya saruji kwa Mkuu wa Mkoa Singida, Dk Rehema Nchimbi kwa ajili ya kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu na afya mkoani humo.

Amesema serikali ya Rais John Magufuli ina dhamira njema na Watanzania na kwamba, inalenga kuhakikisha wanawake wanapata huduma bora kwenye hospitali na vituo vya afya.

Pia, amesema dhamira ya Serikali ni kuona wanafunzi wanapata elimu bora na kwenye mazingira tulivu na rafiki ili kuwawezesha kusoma kwa utulivu.

Mattembe amesema saruji hiyo itagawiwa kwenye shule na vituo vya afya mbalimbali ili kuboresha miundombinu ya majengo ambayo yamechakaa.

“Mheshimiwa Rais wetu anapambana kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na za msingi kama elimu na afya, hivyo sisi wengine ni askari wake wa miamvuli na tuko naye bega kwa bega kuhakikisha tunatimiza malengo kama ilani yetu inavyotuongoza,” amesema Mattembe.