Waombolezaji waaga mwili wa Joyce Mmasi Moshi

Muktasari:

Selasini amesema hakuwahi kumuona hata siku moja Joyce Mmasi akiwa amechukia.

Moshi. Waombolezaji kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro wametoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi, Joyce Mmasi anayezikwa leo.

Shughuli hiyo imefanyika leo Jumatatu Desemba 11,2017 katika Usharika wa Rau wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lililopo umbali wa mita 600 kutoka ilipo Ikulu ndogo ya Moshi.

Miongoni mwa waombolezaji hao ni mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini ambaye alifanya kazi na Joyce tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Wengine ni wanahisa wa kampuni ya Common Link Businesses Ltd ambayo Joyce alikuwa mwanahisa na wanachama wa kundi la Mada Moto (T) na makundi yake dada ambayo alikuwa mwanachama.

Pia, wamejitokeza waandishi wa habari kutoka mkoani Kilimanjaro na mikoa ya jirani, ndugu, jamaa na marafiki.

Mbunge Selasini amesema ilimchukua dakika kadhaa kuamini kuwa Joyce amefariki dunia kutokana na namna alivyoshtushwa na kifo chake.

"Nimemfahamu Joyce akiwa msichana mdogo, wakati huo ndiyo kwanza ameingia kwenye fani ya uandishi wa habari. Sikuwahi kumuona hata siku moja akiwa amechukia," amesema.

Mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni ya Common Link Businesses, Bosco Simba amesema Joyce alikuwa mkereketwa wa maendeleo na ni mwanzilishi wa kampuni hiyo yenye makao yake mjini Moshi.