Mbunge adaiwa kuingilia uchaguzi CCM, mwenyewe aruka kimanga

Muktasari:

  • Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa UWT Wilaya ya Mvomero, Mariam Kambi amemtupia lawama mbunge huyo kuwa alihonga wajumbe ili wamchangue Lidya Mbeaji ambaye alishinda nafasi hiyo.

Katika kile kinachodaiwa kuwa ni kupanga safu ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu 2020, Mbunge wa Mvomero, Suleiman Sadiq amelalamikiwa kutumia fedha kuhakikisha Umoja wa Wanawake (UWT) unaongozwa na watu wanaomuunga mkono.

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa UWT Wilaya ya Mvomero, Mariam Kambi amemtupia lawama mbunge huyo kuwa alihonga wajumbe ili wamchangue Lidya Mbeaji ambaye alishinda nafasi hiyo.

Kambi alisema mbunge huyo ndiye aliyemshawishi Lidya agombee nafasi hiyo na kwamba angemfanyia kampeni ili aweze kushinda.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu madai hayo, Sadiq alisema hajashiriki kwa njia yoyote katika chaguzi za jumuiya zinazoendelea.

“Hizo ni fitina tu za kisiasa, mimi nipange safu ya nini? Safu yangu mimi ni kuwaletea wananchi wangu maendeleo na ndicho ninachofanya,” alisema.

Mbunge huyo alisema anashangaa jina lake kutajwa kwenye uchaguzi huo wakati yeye aliondoka Morogoro tangu Septemba 18, 2017.

Lakini pamoja na utetezi Mariam alidai kuwa, “Tunao ushahidi kwamba mbunge huyu alimfanyia kampeni na kutumia pesa ili kuhakikisha anashinda na kweli ameshinda, lakini hatutaishia hapa kwani hivi naenda kuandaa rufaa.”

Alidai kuwa wapo wajumbe wa mkutano huo ambao walikiri kupewa Sh30,000 na wengine Sh10,000 ili waweze kumchagua mgombea aliyeshinda nafasi hiyo.

“Mbunge ameshiriki sana kuhakikisha Lidya anashinda lakini hakuna shida maana nitakata rufaa hadi haki itendeke, ningeshindwa kihalali wala nisingelalamika,” alisema Mariam.

Julie Bwire ambaye pia aligombea uenyekiti wa UWT wilayani humo alisema chaguzi za jumuiya wilayani humo zilitawaliwa sana na fedha na pia mshindi alianza kampeni kabla ya muda.

“Mimi naandaa rufaa yangu maana uchaguzi huu haukuzingatia kanuni na taratibu tulizopewa maana mshindi ni kama alishapangwa,” alisema.

Licha ya malalamiko na madai hayo, Katibu wa UWT Wilaya ya Mvomero, Zena Minja alisema uchaguzi ulimalizika salama na kwamba baada ya kumalizika ndipo alipoanza kusikia malalamiko ya rushwa.

“Sijapata malalamiko ya maandishi katika suala la rushwa lakini nimelalamikiwa kwa mdomo tu na rushwa kama unavyojua ni ngumu kuthibitisha,” alisema.

Katibu wa UWT Mkoa wa Morogoro, Tuhuma Lihepa alisema hajapokea malalamiko yoyote lakini wagombea wasioridhika wanaruhusiwa kukata rufaa ndani ya mwezi mmoja baada ya uchaguzi.

Katika Uchaguzi huo uliofanyika Septemba 21, nafasi ya Lydia alishinda kwa kupata kura 211 akifuatiwa na Mariam aliyepata kura 122 na Julie kura 47.