VIDEO: Mbunge CUF aibuka na Nondo bungeni

Muktasari:

  • Nondo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam  kwa sasa yupo nje kwa dhamana

Dodoma. Mbunge wa Mgogoni (CUF) Dk Suleiman Ally Yussuf amehoji bungeni leo Jumatatu Aprili 3, 2018 sababu za Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuhoji sababu za kutopelekwa mahakamani kwa muda mrefu.

Nondo anayetuhumiwa kwa makosa mawili kwa sasa yupo nje ya dhamana. Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.

Shtaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareti cha Mafinga.

Alikamatwa Machi 7 na kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Iringa  Machi 26.

Katika swali lake la  nyongeza Suleiman alitaka kujua ni kwa nini Nondo aliwekwa kwa muda mrefu katika kituo cha polisi bila ya kupelekwa mahakamani.

“Sheria gani inatumiwa na polisi kuwaweka mahabusu kwa muda mrefu na watu wanaotuhumiwa kuwa na makosa kama ilivyofanyika kwa kiongozi wa mtandao wa wanafunzi Abdul Nondo,” amehoji Suleiman.

Katika swali la msingi mbunge huyo amehoji ni kwa nini polisi wameshindwa kufanya kazi kwa weledi na kukamata watu pasipokuwa na ushahidi  kwa lengo la kukomoa tu.

Alitaka kujua iwapo kama Serikali haioni haja ya kuwawajibisha watendaji ambao wana tabia ya kuwakomoa wananchi kwa kuwakamata bila kuwa na ushahidi huku akidai anao ushahidi wa waliobambikiziwa kesi ambao ukihitajika anaweza kuwasilisha.

Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema polisi ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa katiba na sheria na linatekeleza majukumu yake kwa mujibu w akatiba.

Amesema polisi wana mamlaka kisheria kutuhumu, kukamata, kuhoji na kuweka watuhumia mahabusu kwa muda ulioruhusiwa kisheria endapo itabainika kuwa kuna viashiria au taarifa ya kuhusika katika kutenda kosa la jinai.

“Kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utendaji zinazoongoza jeshi la polisi inapobanika askari amebambika kesi kwa sababu zozote zile huchukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu ikiwmeo kufukuzwa,” amesema.

Hata hivyo, Mwigulu hakujibu chochote kuhusu Nondo lakini akasema suala la makosa makubwa na ya jinai uchunguzi wake huweza kuchukua muda mrefu zaidi na kuwa kesi zake huwa hazifutwi polisi au mahakamani kwa urahisi.