Mbunge aibua madudu ya JNIA

Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (kulia), akizungumza na Spika wa Bunge, Job Ndugai (kushoto) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Akizungumza wakati wa mahojiano na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mbunge wa Viti Maalumu, (CUF), Riziki Lulida alisema lifti zote zilizopo katika uwanja huo hazifanyi kazi na watu wasioweza kutembea (kama wagonjwa) hubebwa kwenye machela.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), imeshangazwa kubaini abiria wenye mahitaji maalumu kubebwa kwenye machela kutokana na ubovu wa lifti za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mbunge wa Viti Maalumu, (CUF), Riziki Lulida alisema lifti zote zilizopo katika uwanja huo hazifanyi kazi na watu wasioweza kutembea (kama wagonjwa) hubebwa kwenye machela.

“Siku moja nikitokea Marekani, niliona  mtu alikuwa anatokea India alibebwa kwenye machela na watu wanapita pale hakuna cha Scaner (mashine za ukaguzi),” alisema.

Akijibu hoja hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamuriho alisema lifti hizo zinafanya kazi bali kwa siku hiyo  ilikuwa ni bahati mbaya.

“Uwanja umezidiwa na abiria ndiyo maana miundombinu imeharibika, ndiyo maana tumeamua kutengeneza uwanja wa ndege wa Terminal Three,” alisema.

Alisema jukumu la TAA ni katika mashine za ukaguzi kwa wateja wanaoondoka nchini, lakini kwa  upande wa abiria wanaokuja nchini mashine hizo zinasimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

 

“Ndiyo maana siku ile ambayo Rais  alikuta ‘scaner’ hazifanyi kazi  na tuliwaazima za kwetu,” alisema.