Mbunge ampongeza Waziri Mpango kwa kumshughulikia Makonda

Muktasari:

  • Mbunge wa Konde (CUF) Khatib  Said Haji amesema Waziri Mpango alilishughulikia vyema sakata la makontena ya Makonda.

Dodoma. Mbunge wa Konde (CUF) Khatib Said Haji amempongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa jinsi alivyoshughulikia sakata la makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.

Makontena hayo 20 ya samani kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam yanapigwa mnada na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) baada ya maombi ya kusamehewa kodi kukataliwa na Serikali.

Akichangia muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ya mwaka 2018, bungeni leo Septemba 12 2018, Khatib amemtaka Mpango pia kuendelea kumbana hadi haki ipatikane.

“Alizoea kukutana na vingine sasa amekutana cheusi kimemtia doa Rais (John Magufuli anapenda viongozi kama hao,”amesema Khatib.

 

Pia Khatib ametetea uamuzi wa wabunge wa upinzani kukataa bajeti na kwamba mfumo wa kupitisha bajeti hautoi nafasi ya kupambanua wanayoyakubali na kuyakataa.

“Kuna mambo ambayo tunayakubali na kuna tunayoyakataa. Mnafanya dhambi mnaposema maeneo ya wapinzani  wasipewe miradi ya maendeleo kwasababu wamekataa bajeti.

“Kwa mfano wakati tunapitisha bajeti tulisema kuwa kwa kutoza VAT (kodi ya Ongezeko la Thamani) Zeco (shirika la Umeme Zanzibar) Zanzibar inaonewa lakini mkapitisha,”amesema.