Friday, November 10, 2017

Mbunge amtaka mwenzake kuacha kuwashwa washwa

 

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Agnes Marwa amemtaka mbunge mwenzake wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche kuacha kuwashwa washa kwa kuzungumzia masuala nje ya mkoa wake na ajielekeze kuwatetea wananchi wa Nyamongo jimboni kwake.
Agnes anayetoka Mkoa wa Mara pamoja na Heche ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Novemba 10,2017 wakati akichangia mpango wa taifa wa maendeleo wa mwaka 2018/19.
Msemo wa kuwashwa washwa ulitokana na kauli ya Rais John Magufuli katika moja ya hotuba zake Ikulu jijini Dar es Salaam alipowazungumzia viongozi wastaafu akiwataka kutulia na kutozungumzia mambo yasiyo na tija.
Katika mchango wake, Agnes alisema, “Nimemwona mbunge wangu wa Tarime ambako ndiko huko Nyamongo, mheshimiwa Heche yeye anawashwa washwa na uwanja wa ndege ulioko kwa mheshimiwa Rais (Chato mkoani Geita) anashindwa kuwaombea wananchi wetu walipwe fidia zao,” alisema Agnes huku akishangiliwa.
Alisema, “Sasa yeye anatakiwa ajue kwamba wale wananchi wanahitaji yeye awatete si kuwashwa washwa na mikoa mingine kitendo ambacho kwa kweli si kizuri sana na ni kitendo ambacho hakikubaliki hata kidogo.”
“Alitaka uwanja uende nyumbani kwake au ni kosa mheshimiwa wetu Rais kuzaliwa eneo ambalo uwanja wa ndege umepelekwa na ukiangalia kwanza kutokana na mpango suala hili limeangaliwa kwa undani zaidi,” alisema.
Alisema kujengwa uwanja huo Chato kumebana matumizi na ni eneo ambalo kulikuwa na eneo kuliko ungepelekwa mkoani Shinyanga, ungeilazimu Serikali kutumia fedha kulipa fidia wananchi ili kupisha eneo hilo na wananchi wangepata usumbufu.
“Lakini mambo mengine tunapaswa kupeleka siasa mitaani si siasa bungeni… sina mengi zaidi ila nataka mbunge wangu Heche asiwashwe washwe awatetea wananchi wa Nyamongo,” alisema Agnes
Akichangia, mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema kuweka taa za barabarani katika mji wa Chato ni matumizi mabaya ya fedha za umma.
"Tumeona traffic light (taa za barabarani) Chato. Kuna miji ina msongamano wa magari ninyi mnaenda kujenga Chato?" alihoji Matiko.
Alisema Chato haina msongamano wa magari na kuna picha aliona punda wakivuka katika taa hizo japo hana uhakika kama ilikuwa Chato lakini akasema hayo ni matumizi mabaya ya fedha.
Mbali na suala hilo, alisema hata ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege Chato haukustahili bali uwanja wa aina hiyo ungejengwa Dodoma.
Matiko alisema kama uwanja huo  ungejengwa Dodoma, hata ndege kubwa inayombeba Rais wa Marekani, Donald Trump ingeweza kutua badala ya Rais Magufuli kulazimika kwenda Dar es Salaam kumpokea endapo atafanya ziara nchini.
Alisema badala ya Serikali kutumia Sh39 bilioni kujenga uwanja huo, ni vyema fedha hizo zingejenga hospitali kubwa Chato au kujenga chuo kikuu eneo hilo.
Kwa mujibu wa Matiko, Chato kungeweza kujengwa uwanja mdogo ambao utawezesha kutua ndege kama Bombadier na uwanja mkubwa ujengwe Dodoma.

-->