Mbunge atozwa faini kortini kwa fedha ya Uingereza

Muktasari:

Alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke jana akikabiliwa na makosa mawili.

Dar es Salaam. Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea amefikishwa mahakamani kwa kosa la usalama barabarani ambako ametiwa hatiani na kuamriwa kulipa faini kwa Pauni ya Uingereza.

Alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke jana akikabiliwa na makosa mawili.

Mtolea alisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Joseph Maugo kwamba juzi, Julai 19 wilayani Temeke aliendesha gari likiwa na bima iliyokwisha muda wa matumizi.

Katika shtaka la pili, Mtolea anadaiwa kuwa aliposimamishwa na askari wa usalama barabarani alitii lakini akakaidi maagizo ya ofisa huyo.

Mtolea baada ya kusomewa mashtaka hayo aliyakiri yote. Hakimu wa Mahakama hiyo, Eriarusia Nassary alimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Pauni 100 za Uingereza kwa kosa la kuendesha gari ambalo bima yake imekwisha muda wa matumizi.

Katika kosa la pili, alimhukumu kulipa faini ya Sh30,000.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, wakili Hashim Mziray aliyemtetea mbunge huyo katika kesi hiyo alisema alilipa Sh291,000 ambazo ni sawa na Pauni 100 za Uingereza pamoja na Sh30,000 hivyo kufanya jumla kuwa Sh321,700.

Mziray alisema baada ya malipo walikabidhiwa stakabadhi ya Serikali namba 13599087.

Akifafanua kuhusu kutozwa faini kwa fedha ya kigeni, Mziray alisema Sheria ya Bima za Magari ya mwaka 2002, Sura 169 kifungu cha 4(1), 4(2) inasema mtu akikutwa anaendesha gari ambalo bima yake imeisha muda wa matumizi, adhabu ni kifungo cha miezi sita jela au faini ya Pauni 100 za Uingereza.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto alisema mbunge huyo aliyekamatwa juzi, alilala rumande kabla ya kufikishwa mahakamani.

Wabunge wengine kortini

Kufikishwa mahakamani kwa Mtolea jana kunafanya idadi na wabunge wa upinzani waliofikishwa mahakamani katika kipindi kisichozidi siku 20 kwa makosa mbalimbali kufikia watano.

Wabunge wengine ambao wamefikishwa mahakamani katika nyakati tofauti na majimbo yao kwenye mbanao ni Saed Kubenea (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), Cecil Mwambe (Ndanda) na Zubeda Sakuru (Viti Maalumu). Wote ni wabunge wa Chadema.

Julai 5, Kubenea alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kusomewa shtaka la kumshambulia mbunge mwenzake wa CCM, Juliana Shonza nje ya viwanja vya Bunge.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana alidai kuwa mshatakiwa alitenda kosa hilo Julai 3.

Kubenea anayetetewa na mawakili watano, alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa Julai 26.

Julai 20, Mdee alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kumtukana Rais John Magufuli. Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga alidai mbele wa Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa kuwa Mdee alitenda kosa hilo Julai 3.

Alidaiwa akiwa katika makao makuu ya Chadema, alimtukana Rais Magufuli kuwa anaongea ovyo na kwamba anatakiwa afungwe breki.

Baada ya kusomewa mashtaka, Mdee alikana kosa na wakili Katuga alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi itatajwa Agosti 7. Katika mkutano huo, Mdee alikuwa akipinga kauli ya Rais Magufuli iliyopiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba kurejeshwa shuleni baada ya kujifungua.

Julai 17, Sakuru na Mwambe walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na viongozi wengine wa chama hicho wakidaiwa kufanya mkusanyiko bila kibali.

Wakili wa Serikali, Renatus Mkude alisema washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo waliyafanya Julai 15 wilayani Nyasa na kesi yao imepangwa kutajwa Agosti 21.

Nyongeza na Bakari Kiango