Mbunge na DC wa zamani afariki dunia

Muktasari:

  • Ni Danhi Makanga, amepoteza maisha baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda kugongana na bajaji

Mwanza. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Simiyu, Danhi Makanga amefariki dunia leo Jumapili Juni 24, 2018 wilayani Misungwi katika ajali iliyohusisha pikipiki na bajaj.

Taarifa za kifo cha Makanga ambaye amewahi kuwa mkuu wa wilaya na mbunge zimethibitishwa na mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda.

Sweda ameieleza MCL Digital kuwa ajali hiyo imetokea leo asubuhi eneo la Nyashishi na kwamba marehemu alikuwa amepanda pikipiki iliyogongana na bajaji na kusababisha kifo chake na dereva wa pikipiki hiyo.

"Ni kweli ajali imetokea na wote wawili wamefariki ila dereva wa bajaji amepata majeraha. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospital ya wilaya ya Misungwi, "amesema Sweda.