Mbunge wa CCM Manyoni kusota rumande hadi kesho

Muktasari:

Mtuka anatarajiwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Manyoni kujibu tuhuma za kumgonga mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Sukamahela, Salome Paschal (10) na kusababisha kifo chake.

Singida. Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Daniel Mtuka (51) anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi hadi kesho atakapofikishwa mahakamani.

Mtuka anatarajiwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Manyoni kujibu tuhuma za kumgonga mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Sukamahela, Salome Paschal (10) na kusababisha kifo chake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magilingimba alisema kwa kuwa jana ilikuwa Jumamosi ambayo sio siku ya kazi, wamelazimika kusubiri hadi kesho watakapomfikisha mahakamani.

“Mahojiano na mtuhumiwa Mtuka yameshakamilika, lakini kwa vile mahakama leo (jana) haifanyi kazi, tutamfikisha Jumatatu,” alisema Kamanda Magilingimba.

Imedaiwa kwamba Agosti 10, saa 8:35 mchana, mbunge huyo akiwa njiani kwenda jimboni kwake akitokea Dodoma mjini akiwa anaendesha gari aina ya Toyota Prado, alimgonga mwanafunzi huyo aliyekuwa akivuka kutoka upande wa kulia kwenda kushoto mwa barabara.

Kamanda Magilingimba, alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva Mtuka kushindwa kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.