Thursday, September 14, 2017

Mbunge wa CCM aeleza alivyohusika ndege iliyomsafirisha Lissu

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi

Dodoma. Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky ameeleza alichokifanya katika suala la ndege iliyomsafirisha Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ni kuingia dhamana na si kulipa malipo taslimu ya dola 9,000 za Marekani.

Turky alimesema hayo leo Alhamisi mara baada ya kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa alilipia gharama za ndege hiyo.

Amesema kuwa nyaraka inayosambaa katika mitandao ya jamii inayosemekana kutumwa na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Peter Msigwa sio tiketi ni invoice.

Amesema anapenda kuiweka Tanzania katika hali ya usalama na ukweli na kwamba maneno mengine si vizuri.

“Tusifanye tukio la Tundu Lissu kuwa la siasa. Mimi binafsi tukio zima la mbunge mwenzangu limenisikitisha sana limenisononesha sana. Nikiwa kama kamishna wa Bunge lakini pia ni binadamu kuna kuzaliwa na kufa,”amesema.

“Kwa hiyo tukio hilo lilipotokea tuliitwa na makamishna wote na Spika wetu wakiwemo Mbowe (Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani) Msigwa na timu yake. Kwanza ndege ilikuwepo pale Airport ambayo ilikuwa imeshaagizwa na Bunge iko stand by kumpeleka moja kwa moja Muhimbili.”

Amesema walichoamua ni kuwa aende moja kwa moja Nairobi nchini Kenya lakini ndege hiyo haikuwa na kibali cha kwenda nchini humo na kwamba ili uweze kwenda nchini humo unalazimika kuwa na marubani wawili.

Hata hivyo, amesema Spika Ndugai alihangaika kupata kibali cha ndege iliyokuwepo uwanjani ili iweze kumpeleka mgonjwa Nairobi.

“Wakati mambo yote tayari rubani wa ndege akasema kuna kitu kinaitwa landing Instrument ambayo ile ndege haina kwa hiyo haitaweza kuruka,” amesema.

Amesema kutokana na majibu hayo waliingiwa na sitofahamu watafanya nini lakini yeye aliingia katika uzoefu wake aliopewa na Mungu kwa kutafuta ndege kwa ndugu zake ambao wanafanya nao biashara sana.

“Nikawaambia ndege ipo wakatoa nauli zao za ghali ghali kwa sababu tunajuana wakakubali kutusaidia kwa dola 9,200 pamoja na ambulance (gari la wagonjwa) mimi ndio niliyoita kwa kubaliana na Mbowe na Msigwa kwamba Turky haya mambo yasimamie baadaye…na ndicho

kilichofanyika,” amesema.

Amesema ilikuwa siku ya pili walipe fedha hizo lakini haikuwezekana na kwamba jambo hilo limezungumziwa bungeni na Spika kuwa yeye ametoa fedha hizo na kwamba Chadema watalipa.

Amesema kauli hiyo haina tatizo kwa sabababu kama Chadema isingelipa hadi jana ingebidi atoe fedha zake kulipa deni hiyo la ndege.

“Kwa sababu wale mabwana watakuwa wamepitiliza bahati leo mchana nimempigia mwenye ndege saa 6.30 ndio akaniambia kuwa wamelipa,”amesema.

Alipoulizwa kwa maana hiyo yeye aliingia udhamini wa malikauli, Turky

amesema malikauli hiyo kwake inakubalika si kwa mtu mwingine.

Amesema malikauli iliyokuwa inahitajika pale ni kwamba kama Chadema wasipolipa basi papatikane mtu wa kulipa.

“Hapana sikulipa cash(fedha taslimu) na bahati mbaya siku ile

isingeweza kuruka kama zisingepatikana dola 9000 kwa maana lazima ulipe ndio ndege iruke na hapa Dodoma hakuna mtu aliyekuwa na hata dola 1000 kwa hivyo ilikuwa kidogo hali ngumu lakini tunamshukuru Mungu nia njema hufungua milango yake,”amesema.

Alipoulizwa kama ana hisa katika kampuni hiyo, Turky amesema hana hisa na kwamba ndege hizo amekuwa akizutumia mara nyingi .

-->