Wednesday, May 23, 2018

Mchakato kwa diaspora kuchangia uchumi wa Taifa waanza

 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Susan Kolimba amesema wizara hiyo imeanza kuandaa sera ya Taifa ya jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni (diaspora ) ili waweze kuchangia uchumi wa nchi.

Akizungumza bungeni leo Jumatano Mei 23, 2018 mjini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, Dk Kolimba amesema wizara imeunda timu ya kuandaa sera hiyo.

“Timu hii itaainisha  mikakati na kutoa mwongozo kuhusu ushiriki wa diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi,” amesema Dk Kolimba.

Amesema wizara hiyo imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2018/19 na  imeanza mchakato wa kukamilisha sera ya mambo ya nje ya Tanzania na kuongeza kuwa kwa sasa wanaandaa mkakati ambao ukikamilika utapelekwa kwa wadau.

Kuhusu wafungwa 11 walioko nchini Msumbuji, Dk Kolimba ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), amesema wamewasiliana na balozi wa Tanzania nchini Msumbiji ili kuhakikisha masilahi yao yanalindwa.

Dk Kolimba akigusia suala la upatikanaji wa fedha za ujenzi wa makazi na ofisi za balozi za Tanzania nje ya nchi, kubainisha kuwa wanafuatilia fedha katika Wizara ya Fedha na Mipango ili kukamilisha jambo hilo.

 


-->