Mchakato wa kuiibua Mv Nyerere waanza

Muktasari:

Kazi hiyo inayofanywa na kampuni ya Songoro Marine chini ya usimamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), inatarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja.

Dar es Salaam. Wazamiaji na wataalamu mbalimbali jana wameanza kazi ya kukinyanyua kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Alhamisi iliyopita na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 224.

Kazi hiyo inayofanywa na kampuni ya Songoro Marine chini ya usimamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), inatarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Kijiji cha Bwisya Kisiwa cha Ukara kilipozama kivuko hicho, mtaalamu kutoka kampuni hiyo, Meja Songoro alisema hatua ya kwanza itakuwa kuingiza hewa ndani ya kivuko ili kuyatawanya maji na kuanza kukivuta.

“Kivuko kinaendelea kuelea kwa sababu kuna hewa ndani yake. Wakati kinageuka (kupinduka) kilichota maji, tutaanza kuingiza hewa kutoa maji na kuanza kukivuta. Tutakapoanza kuyatawanya maji hayo, pia tutapeleka boya na hii itafanya chombo kizidi kuja juu. Baada ya hapo tutakisogeza taratibu hadi kwenye maji mafupi.”

Alisema baada ya hatua hizo kitu kitakachofuata na kuingiza pampu za maji kwa ajili ya kuyaondoa maji yote na ndipo chombo hicho kitageuka na kuanza kuelea katika hali ya kawaida.

Mtaalamu huyo alimhakikishia Majaliwa kufanya kazi hiyo kwa weledi, “Tutakuwa makini na ni matumaini yetu tutafanikiwa.”

Baadaye Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alisema kazi hiyo inatarajiwa kufanyika kwa muda mfupi zaidi baada ya baada ya kuwasili kwa kifaa maalumu kitakachotumika kukipindua kivuko hicho. “Kivuko hiki kimejikita chini na kifaa hiki kitaingiza upepo utakaoingia kwenye maboya yatakayosaidia kukipindua na hatua ya kukipindua itasaidia kivuko hiki kutoharibika,” alisema.