Mchanga wa madini wawaibua Kaiza, Mbowe

Muktasari:

Kaiza alisema jana kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya kuchunguza mchanga wa madini iliyowasilishwa siku chache zilizopita ni wazi kampuni hizo hazikuwa zikitoa taarifa sahihi kwa Teiti.

Dar/Dodoma. Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa na hofu huenda kitendo cha Tanzania kuzuia makontena ya dhahabu kikaliingiza Taifa matatani katika mahakama za kimataifa, aliyekuwa mjumbe wa Mpango wa Uhamasishaji wa Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti), Bubelwa Kaiza amesema ipo haja ya kupitiwa upya kwa taarifa za fedha za kampuni za madini ambazo zilikuwa zikiwasilishwa kwao.

Kaiza alisema jana kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya kamati ya kuchunguza mchanga wa madini iliyowasilishwa siku chache zilizopita ni wazi kampuni hizo hazikuwa zikitoa taarifa sahihi kwa Teiti.

Alisema Teiti ilikuwa inapitia taarifa za fedha ambazo zilikuwa zinawasilishwa kwa hiari na kampuni husika na sio kuchunguzwa, hivyo upo uwezekano walikuwa wanatumia mwanya huo kutoa taarifa za uongo.

Kaiza alisema kwamba, katika taarifa walizokuwa wanapewa na kampuni hizo mara nyingi zilijikita katika hesabu, lakini hakukuwa na maelezo yoyote ya namna makinia yalivyokuwa yakiziingizia fedha nyingi.

Awali, akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Chadema mjini Dodoma jana, Mbowe alisema kuna tetesi kuwa uchunguzi huo ambao ulimng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo una upungufu mwingi.

“Tanzania inaruhusu kupitishwa kwa sheria mbovu na wizi halafu baadaye wanapiga kelele, wapinzani tunasema sheria zote lazima zifumuliwe na kupangwa upya,” alisema