Mchimbaji mdogo Mererani anusurika kufa baada ya kuchomwa moto

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Masawe akizungumza na Mwananchi  leo (Jumatano)amesema tukio hilo, limetokea juzi saa tatu usiku katika mgodi unaomilikiwa na Nickson Emmanuel katika machimbo ya Tanzanite Mererani.

 Mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite Mererani, Joel Ephata(34) amenusurika kufa baada ya kuchomwa moto na wamiliki wa mgodi anaofanya kazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Masawe akizungumza na Mwananchi  leo (Jumatano)amesema tukio hilo, limetokea juzi saa tatu usiku katika mgodi unaomilikiwa na Nickson Emmanuel katika machimbo ya Tanzanite Mererani.

Amesema mchimbaji huyo, mdogo amechomwa moto maeneo mbali mbali ya mwili wake, baada ya kutuhumiwa kuhusika na upotevu wa vifaa katika mgodi huo.

"Tumeanza uchunguzi wa tukio hili, tayari tumemkamata mmiliki wa mgodi huo, Nickson Emmanuel, kwa mahojiano ili awataje wenzake waliohusika na uchunguzi ukikamilika tutawafikisha mahakamani," amesema.

Kamanda Masawe amesema Ephata ambaye alikuwa amelazwa kituo cha afya Mererani, alitarajiwa kuhamishiwa hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa matibabu zaidi.

 

Akizungumzia tukio hilo leo, Diwani wa Kata ya Mererani, Thobias Obero amesema matukio ya kunyanyaswa wachimbaji wadogo na waajiri wao, yanapaswa kukomeshwa.

 

 

Obero aliomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa tukio hilo na wahusika wafikishwe mahakamani ili kukomesha matukio hayo.

 

Wakizungumzia tukio hilo, Edna Momo na Elizabeth Nanyaro, waliiomba Serikali kuingilia kati kutetea maslahi ya maelfu ya wachimbaji wadogo ambao wengi ni vibarua na hawana hata mikataba.

 

Momo alimuomba Rais John Magufuli, kuingilia kati ili kuhakikisha haki za maelfu ya wachimbaji wadogo zinapatikana kwani wanaonufaika na madini ni wachimbaji wenye migodi pekee.

 

"Rais njoo Mererani kuna majipu huku, watu wanamiliki migodi wanapata mamilioni ya fedha lakini hawawalipi watu wanaochimba na wala hawana mikataba nao," amesema.