Mchungaji aililia Sumatra

Muktasari:

Ameiomba Sumatra isiwazuie kuhubiri kwenye kwenye mabasi kwa kuwa hawachukui dakika nyingi

Dar es Salaam. Baadhi ya wachungaji wanaotoa huduma za kiroho katika magari yaendayo mikoani wameiangukia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa kuitaka kutafakari upya uamuzi wa kuwazuia kufanya shughuli hiyo.

Hivi Karibuni Sumatra ilipiga marufuku kwa wafanyabiashara na wahubiri kufanya shughuli ndani ya mabasi ya abiria na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka agizo hilo.

Lakini Leo , Novemba 17 mmoja wa wachungaji hao aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Joseph Hongoa anayetoa huduma hizo katika kituo cha mabasi cha Ubungo, akizungumza na gazeti hili kwa niaba ya wachungaji wenzake sita wanaiomba Sumatra kutafakari na kujiridhisha kama kuna madhara  na usumbufu unaojitokeza wakati wakitoa huduma hiyo.

“Jambo hili limetustusha sana, kwa sababu tunachokifanya ni kuombea abiria ili wasafiri salama na huu ndiyo ubinadamu unaotakiwa. Pia maombi yetu yanasaidia kuwarudisha katika misingi ya maadili miongoni mwa abiria wanaokuwamo katika magari haya,”amesema Mchungaji Hangao.

Amesema hivi sasa maadili yanazidi kumomonyoka na neno la Mungu ni njia ya pekee ya kuwarudisha Watanzania kwenye misingi bora ya bora inayotakiwa katika maisha ya kila siku.

“Sidhani kama ni kero kwa sababu huwa hatutumii dakika nyingi ni 10 hadi 15. Ndiyo maana tunaiomba Sumatra itafakari ikiwezekana ituite na tukae pamoja kwa ajili ya majadiliano kuhusu suala hili,”amesema Mchungaji Hangao.

Juzi kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Leo Ngowi alinukuliwa kituo cha runinga cha Azam akisema hatua hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za sheria mpya za Sumatra baada ya abiria kulalamika shughuli hizo zimekuwa kero wakiwa kwenye vyombo vya usafiri.

“Kanuni imekataza kufanya mikutano, siyo la watu kujadiliana. Kwa mfano amesoma katika gazeti jambo fulani na amekaa na mwenzake kisha kuanza kujadiliana hili linaruhisiwa. Lakini mtu mmoja kulazimisha watu kukaa kimya katika gari na kuanza kuhubiri hili limekatazwa.

“Kimsingi watu wengine hawahitaji kujua hayo na kanuni imezingatia hilo.Tunaomba umma wa Watanzania waendelee kupata elimu kutoka Sumatra.

Ngowi amesema kwa mujibu Sheria hizo mpya, adhabu zake zimeganyika katika aina mbalimbali ikiwamo kutoa onyo kwa watu watakaobainika kukiuka marufuku hiyo.