Mchungaji anayedaiwa kuvuliwa nguo na polisi wanne ajieleza upya

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita.

Muktasari:

Habari zilizopatikana jana zimesema kwamba polisi walifanikiwa kumpata mchungaji huyo juzi baada ya kumtafuta kwa karibu wiki mbili, bila mafanikio kutokana na simu yake kuzimwa.

Moshi. Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) anayedaiwa kuvuliwa nguo na polisi wanne kisha kupigwa picha akiwa na mtu mwingine kwenye nyumba ya wageni limechukua sura mpya baada ya kulazimika kuandikisha maelezo upya juu ya tukio hilo kwa kuwa ya awali aliyoyatoa polisi yametofautiana na alivyojieleza mbele wakuu wa vyombo vya kiuchunguzi.

Habari zilizopatikana jana zimesema kwamba polisi walifanikiwa kumpata mchungaji huyo juzi baada ya kumtafuta kwa karibu wiki mbili, bila mafanikio kutokana na simu yake kuzimwa.

Katika maelezo yake kwa wakuu wa vyombo vya uchunguzi, mchungaji huyo alidai kutengenezewa tukio la ushoga kwa kuvuliwa nguo kwa nguvu akiwa na mtu mwingine, kupigwa picha na kutakiwa kutoa fedha.

Maelezo ya awali yalidai kwamba watu waliomfanyia kitendo hicho walikuwa ni polisi wanne, ambao walimtaka atoe Sh10 milioni ili wamwachie na kuzima tukio hilo. Hata hivyo, hakuwa na fedha hizo lakini akafanikiwa kuwapa Sh5.4 milioni ambapo walimwachia na ndipo alipotoa taarifa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Polisi.

Lakini ilidaiwa kuwa alipokabidhiwa polisi ili aandikishe maelezo, alitoa taarifa zilizotofautiana ya awali, jambo ambalo liliwashtua maofisa wa Takukuru na Polisi.

Hali hiyo ndio iliyosababisha kutolewa kwa amri mchungaji huyo kutafutwa upya ili kuandika maelezo sahihi kuhusiana na kile kilichomtokea.

Jana, Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema mchungaji huyo amesharekebisha maelezo yake na hawana ugomvi naye kwa kuwa upungufu uliokuwapo ameshaujazia.

“Nafikiri kwenye mahojiano yake ya awali hakuhojiwa vizuri. Mapungufu tuliyoyagundua kwenye maelezo yake ya awali ameshayaondoa na sasa tunaendelea naye vizuri,” alisema.

Polisi bado inaendelea kuwashikilia askari wake wanne wa wilayani Hai wanaodaiwa kutengeneza tukio hilo kwa lengo la kujipatia fedha huku wakimsaka mtu anayedaiwa kutengenezwa kumghilibu mchungaji.