Mdahalo wa aina yake; Clinton,Trump wachuana vikali

Muktasari:

Jana wamepambana vikali katika mdahalo wa kwanza wa televisheni ambapo wamepingana katika masuala mbali mbali ikiwamo masuala ya sera, kodi, ajira na uchumi.

Mdahalo wa kwanza na wa aina yake baina ya wagombea urais nchini Marekani Hillary Clinton na Donald Trump jana ulitazamwa na watu zaidi ya 100 milioni huku kura za maoni zikionyesha wawili hao wanakaribiana katika uungwaji mkono.

Jana wamepambana vikali katika mdahalo wa kwanza wa televisheni ambapo wamepingana katika masuala mbali mbali ikiwamo masuala ya sera, kodi, ajira na uchumi.

Kura za maoni zinaonyesha wawili hao wanakaribiana sana katika uungwaji mkono.

Kadhalika wamejibizana kuhusu Vita vya Iraq na juhudi za kukabiliana na kundi linalojiita Islamic State.

Msimamizi wa mdahalo huo uliorushwa na kituo cha Televisheni cha CNN, Lester Holt amemwuliza mgombea wa chama cha Republican Donald Trump mbona  bado hajaweka wazi taarifa zake za ulipaji kodi.

Mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton amemshutumu mpinzani huyo wake akisema amekuwa akikwepa kulipa kodi na kudokeza kwamba hilo lina maana kwamba hakuwezi kuwa na wanajeshi, pesa za kulipa wanajeshi waliostaafu pamoja na kufadhili elimu na huduma ya afya.

Lakini tajiri huyo kutoka New York amejibu kwa kusema kwamba atatoa hadharani taarifa hizo iwapo  Clinton naye atakubali kutoa barua pepe 33,000 ambazo zilifutwa kutoka kwa kwenye akaunti yake wakati wa uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba alitumia barua pepe ya kibinafsi kwa kazi rasmi alipokuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani.

 Clinton amekubali lawama kuhusu kosa hilo na kusema hana na "kisingizio".

Kadhalika,  Trump amemlaumu mpinzani wake huyo kuhusu kupotea kwa ajira akisema nafasi za kazi "zinaikimbia nchi" na akalaumu mikataba duni ya kibiashara.

Trump alisema Clinton ni  "mtu wa maneno mengi, bila vitendo".

Clinton ameahidi kuongeza uwekezaji na kuahidi kuunda nafasi takriban 10 milioni za kazi.

Mambo mengine makuu yaliyoibuka kwenye madahalo:

  • "Umekuwa ukikabiliana na ISIS maisha yako yote,'' Trump amemkejeli Bi Clinton
  • Amesema Bi Clinton hana uwezo wa  kudhibiti ukali wa kumuwezesha kuwa rais.
  • Wamarekani Weusi wanaishi "katika jehanamu" nchini Marekani, Trump amesema, kwa sababu maisha yao yamekuwa hatari sana.
  • Akijibu kupigwa risasi kwa watu weusi, Trump amesema suluhu ni kurejesha utawala wa sheria.

Clinton amesema akichaguliwa kuwa rais atatekeleza mageuzi katika mfumo wa sheria kwa sababu "suala la asili limekuwa likiamua mengi".

 Kwa taarifa hii zaidi na nyingine nyingi  nunua gazeti lako la Mwananchi kesho au soma mtandaoni BONYEZA HAPA