Mdogo wa marehemu Akwilina apelekwa Tanga kusoma

Muktasari:

  • Angela alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Maki iliyopo Tarafa ya Mashati, wilayani Rombo.

Rombo. Hatimaye Angela Akwilini ambaye ni mdogo wake na aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini amechukuliwa jana nyumbani kwao kwenda kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Wasichana Korogwe jijini, Tanga.

Angela alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Maki iliyopo Tarafa ya Mashati, wilayani Rombo.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyoitoa kwa Angela Februari 23, wakati wa maziko ya marehemu Akwilina aliyeuawa Februari 16, kwa kupigwa risasi na akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa Familia, Dismas Shirima alisema mwanafunzi huyo alichukuliwa jana kwa ajili ya kupelekwa shule aliyopangiwa na Waziri Ndalichako.

“Sisi kama familia tumechukulia jambo hili kama mojawapo ya mafanikio ambayo Waziri Ndalichako alituahidi kwamba hataiacha familia hii hivi hivi” alisema Shirima.

“Hatua zote za kumchukua Angela zilikuwa wazi na sisi familia tumepewa mawasiliano na jana viongozi wa Serikali walimkabidhi mwalimu anayempeleka Angela moja kwa moja hadi Shule ya Korogwe,” aliongeza.

Pia, Shirima alisema Waziri Ndalichako ameahidi kwenda kumchukua mdogo wake mwingine Akwilina, Yulia Akwilini aliyeacha shule akiwa kidato cha tatu kwa kukosa mahitaji ya shule ili kupelekwa chuo kwa ajili ya kujiendeleza kielimu.

“Waziri ametuambia kuna taratibu anakamilisha za kuja kumchukua Yulia ili aendelee na shule ya ufundi, kwa hiyo amesema taratibu zikikamilika atakuja tena kumchukua,” alisema.