Meghji aitaka MOI kutengeneza mbinu za kimkakati

 Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini Taasisi ya Mifupa Muhimbili Zakia Meghji

Muktasari:

  • Wajumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) leo wamekutana kupitia na kupitisha mikakati na mipango mbalimbali inayolenga kuboresha huduma kwa wagonjwa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Zakia Meghji amesema taasisi hiyo ni tegemeo kubwa kwa Watanzania na nchi nyingi za Afrika hivyo ni muhimu kuendelea ketengeneza mbinu za kimkakati za kuendelea kutoa huduma bora.

Meghji amesema hayo leo Oktoba 8, 2018 wakati akiongoza wajumbe wa bodi hiyo kupitia na kupitisha mikakati na mipango mbalimbali inayolenga kuboresha huduma kwa wagonjwa kuelekea maadhimisho ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano.

Amesema kuanzisha huduma mpya za matibabu na kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha huduma zote za afya zinapatikana nchini na hivyo kufuta rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi ambazo zimekuwa zigharimu Serikali fedha nyingi.

“Nafahamu sasa tunakwenda vizuri, Serikali imetuwezesha tumekuwa na vifaa vya kisasa kabisa, tuna MRI ya kisasa sawa na ile inayotumika huko ulaya, tuna CT SCAN ya kisasa pia,tuna X-ray za kidigitali hivyo ni muhimu kuendelea kujipanga kuboresha huduma zetu. Naamini MOI ni bora lakini ni lazima kuboresha zaidi,”amesema.

Amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kimepitia taarifa ya mfumo wa upimaji wa wazi wa watumishi yaani OPRSAS pamoja na masuala mengine yanayolenga kuboresha huduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface amesema MOI iko kwenye mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma zake hapa barani Afrika ambapo siku za hivi karibuni wananchi wengi kutoka mataifa jirani wamekuwa wakifika kupata huduma, hivyo lazima huduma ziboreshwe ili waendelee kupata huduma stahiki na kwa wakati.

“Ni ukweli usiopingika kwamba, huduma zetu zimeboreka sana katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na John Magufuli, tuna vifaa vya kisasa kabisa hivyo ni muhimu sisi viongozi kukutana na kuhakikisha tunaboresha huduma kadri iwezekanavyo,” amesema Boniface.

Amesema MOI imepata vifaa vya kisasa hivyo ni muhimu kukutana na kutengeneza mikakati  ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kwa kuleta wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ili huduma zote ziendelee kutolewa hapa nchini.

Amesema hivi karibuni taasisi itakuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la madaktari wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

Vikao vya bodi ya wadhamini MOI vimekuwa vikifanyika kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya utoaji huduma na kuhakikisha changamoto zote zilizojitokeza katika kipindi hicho zinatatuliwa.