Mengi aomba kujitetea kwa kiapo asifungwe

Muktasari:

Mengi alitoa maombi hayo jana kupitia kwa wakili wake, Deogratius Ringia baada ya amri ya Mahakama hiyo iliyotolewa na Jaji Mfawidhi, Amir Mrumi, Agosti 9, mwaka huu, ikimtaka afike mahakamani hapo jana kujieleza kwa nini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza hukumu hiyo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi ameiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara kuwasilisha utetezi kwa njia ya kiapo ya kwa nini asifungwe jela kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya Mahakama hiyo katika kesi ya ununuzi wa hisa.

Mengi alitoa maombi hayo jana kupitia kwa wakili wake, Deogratius Ringia baada ya amri ya Mahakama hiyo iliyotolewa na Jaji Mfawidhi, Amir Mrumi, Agosti 9, mwaka huu, ikimtaka afike mahakamani hapo jana kujieleza kwa nini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza hukumu hiyo.

Mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Aghaton Nchini na kusomwa katika kesi ya msingi ya madai iliyofunguliwa na wafanyabiashara watatu, ilimwamuru Mengi kuwalipa jumla ya Sh1.2 bilioni.

Licha ya Wakili Ringia kukanusha kwenye vyombo vya habari kuwa Mengi hahusiki katika kesi hiyo aliyotakiwa kufika mahakamani kujitetea kwa nini asifungwe, jana wakili wake huyo alifika mahakamani hapo na kudai  mteja wake ameshindwa kufika kwa sababu anaumwa.

Pamoja na kuiarifu Mahakama kuwa Mengi ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa na yuko kwenye mapumziko, aliiomba Mahakama impe siku 14 ili aweze kuwasilisha kiapo chake cha utetezi, madai ambayo yalipingwa na wakili wa wadai, Mafuru Mafuru.