Meya awataka wahandisi kufanya tathmini ya ujenzi wa barabara

Muktasari:

  • Wananchi wametakiwa kuacha kutiririsha maji machafu kwenye barabara kwani kufanya hivyo kunazifanya ziharibike haraka

 Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam Boniface Jacob amewaagiza wahandisi wa halmashauri hiyo kufanya tathmini ya gharama za matengenezo ya Barabara ya Kilimahewa-Kwamloka-Tiptop.

Barabara hiyo ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu kwa sababu ya ubovu.

Jacob ametoa agizo hilo leo Ijumaa Julai 28 akiwa kwenye ziara ya Kamati ya Uchumi na Fedha ya Halmashauri hiyo, iliyofanywa kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata ya Makurumla, Manispaa ya Ubungo na kuona namna ya kuzitatua.

Akizungumza katika ziara hiyo, Meya huyo amesema ubovu wa barabara uliosababisha mashimo makubwa kutokana na mvua kuliwafanya wananchi wa eneo hilo kushindwa kuitumia barabara hiyo kwa muda mrefu.

“Tumekubaliana kwamba wahandisi wanatakiwa kufika na kuifanyia tathmini barabara hii ili irejee kwenye hali yake ya awali, wananchi waanze kuitumia,”amesema.

Meya huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha, aliwataka wananchi kutotiririsha maji machafu kwenye barabara ili kuzifanya zidumu na kutumika kwa muda mrefu.

“Barabara hii ya Mtaa wa Kwa Jongo-Mianzini imeathirika zaidi na maji machafu, wananchi wana jukumu la kutunza barabara hizi,”amesisitiza.