Meya wa Ukawa aungana na Rais John Magufuli

Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kwiyeko akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo. Picha na Salim Shao 

Muktasari:

Wamachinga katika ya jiji hawapaswi kuhamishwa mpaka watakapopatiwa maeneo mbadala.

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko (Chadema), ameungana mkono na Rais John Magufuli, kuwakingia kifua wafanyabiashara wadogo maarufu Wamachinga akitaka wasibughudhiwe na mtu yeyote.

Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari, Kuyeko alisema wafanyabiashara hao waendelee kufanya shughuli zao katikati ya jiji.

“Machinga waendelee kufanya kazi bila bugudha. Kusiwe na mtu yeyote wa kuwasumbua,” alisema.

Kauli hiyo ya Kuyeko inaweka mkazo kwenye kauli aliyoitoa Rais Magufuli hivi karibuni alipokuwa ziarani jijini Mwanza alipotengua mpango wa kuwaondoa Machinga katikati ya Jiji la Mwanza uliokuwa umepangwa kutekelezwa Agosti.

Badala yake, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa jiji hilo kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa na mbunge wa Nyamagana, kushirikiana kuandaa maeneo ya kuwapeleka Wamachinga hao badala ya kuwaondoa huku kukiwa hakuna maeneo mbadala yaliyotengwa kwa ajili ya wao kufanyia biashara.

Meya huyo alisisitiza kuwa Rais Magufuli ni Rais wa Watanzania wote, haijalishi kauli hiyo aliitolea sehemu gani, bali inatosha kutambua tu kuwa aliwasemea wamachinga wote wakiwamo wa Jiji la Dar es Salaam. “…Waendelee kukaa mjini kufanya biashara hadi baraza la madiwani litakapo kaa (tarehe itapangwa) na kuamua maeneo watakayopangiwa kwa ajili ya wao kufanyia biashara. Kutoa kauli za kuwataka leo waondoke na kurudi ni kuwachanganya.”

“Wamsikilize nani wamuache nani. Rais Magufuli ameshasema waendelee kufanya biashara katikati ya jiji hadi mpango wa kuwapatia maeneo yao utakapokamilika,” alisema.

Msisitizo wa kauli ya meya huyo ya kuwakingia kifua Machinga, unalenga kuwaondoa hofu wafanyabiashara hao ambao walianza kuingiwa na wasiwasi baada ya Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaondoa katika maeneo ya Soko la Kariakoo na barabarani, hususan karibu na barabara za mabasi ya mwendo kasi.

Kupitia agizo hilo alilolitoa hivi karibuni, Simbachawene alisema kurejea kwa wafanyabiashara katika maeneo hayo kumeleta usumbufu na uchafu wa mazingira katika maeneo mengi ya jiji, hivyo Makonda asilegeze kamba katika suala hilo.