Meya wa zamani Dar afariki dunia

Muktasari:

  • Kleist Skyes alikuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam mwaka 2000 hadi 2005.

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Kleist Sykes amefariki dunia.

Familia imesema Sykes amefariki dunia leo Jumatano Novemba 22,2017 asubuhi na mipango ya mazishi inaendelea kufanyika.

Skyes aliyekuwa meya mwaka 2000-2005 amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan.

Mwanamuziki wa kizazi kipya, Dully Sykes ambaye Kleist ni baba yake mkubwa akizungumza na Mwananchi amesema meya huyo wa zamani amefariki dunia leo saa mbili asubuhi.

“ Yaah, kweli amefariki na sasa familia tumeanza kukutana kujua mazishi yatafanyika lini,” amesema.

Meya wa sasa wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita akizungumza na Mwananchi amesema hivi karibuni alimtembelea hospitalini alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na tatizo la moyo.

Mwita amesema kuna wakati Sykes alimtembelea ofisini kwake na alimpa ushauri kuhusu utendaji kazi.

“Ni mtu tuliyeelewana, amewahi kuja hapa ofisini kwangu kama mara mbili na kunishauri haya na yale kuhusu kazi zangu,” amesema.

Kleist Sykes aliyekuwa diwani wa Kivukoni mwaka 2000 hadi 2005 anatoka katika familia ambayo ni miongoni mwa zenye wanasiasa walioshiriki katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.