Mfalme Saudia awafuta makamanda wa jeshi

Muktasari:

Kwa mujibu wa amri ya kifalme iliyotolewa Jumanne waliofukuzwa ni pamoja na mnadhimu mkuu wa jeshi na wakuu wa vikosi vya ardhini na anga.

 Mfalme Salman wa Saudi Arabia amewafuta kazi makamanda wa ngazi ya juu wa jeshi na amebadili Baraza la Mawaziri katika hatua iliyotingisha vyombo muhimu vya usalama na wizara za serikali.

Kwa mujibu wa amri ya kifalme iliyotolewa Jumanne waliofukuzwa ni pamoja na mnadhimu mkuu wa jeshi na wakuu wa vikosi vya ardhini na anga.

Luteni Mkuu Fayyad bin Hamed al-Ruwayli aliteuliwa kuwa mnadhimu mkuu. Tamadur binti Youssef al-Ramah aliteuliwa kuwa naibu wa waziri wa kazi nafasi ambayo ni mara chache kupewa wanawake katika ufalme.

"Yeye (Mrithi wa Ufalme Mohammed bin Salman) ndiye mtu anayeendesha nchi kwa sasa. Hakuna shaka yoyote kuhusu hilo," alisema James Dorsey, mwanazuoni katika chuo cha S Raja Ratnam, Singapore.

"Inafaa kukumbuka kwamba kwa hakika mkuu huyo amebadilika kabisa muundo wa serikali ya Saudi Arabia," alisema na akaongezea kuwa ni utawala wa mtu mmoja kinyume na siku za nyuma wakati maamuzi yalifanywa kwa makubaliano.

"Nafikiri tutaona mabadiliko zaidi kwa wafanyakazi ndani ya jeshi na pia utawala wa kiraia tu kwa sababu tu anaweka watu wake na anataka kuunda picha fulani ya ufalme."

Hakuna sababu rasmi iliyotolewa kutokana na mabadiliko haya, lakini yanakuja wakati huu Saudi Arabia inakabiliwa na ongezeko la shutumu juu ya kuhusika kwake katika vita nchini Yemen.

Muungano wa majeshi yanayoongozwa na Saudi Arabia ulianzisha mashambulizi Machi 2015 baada ya waasi wa Houthi kuutwaa mji mkuu, Sanaa na kuzingira eneo kubwa la nchi masikini mapema mwaka uliopita.