Mfanyabiashara ajilipua mbele ya bosi wa TRA

Muktasari:

  • Amesema wafanyabiashara wamechoshwa na tabia ya kupandishiwa makadirio ya mapato kila mwaka na wameshatoa malalamiko kwenye vikao mbalimbali hiyo bado hawasikilizwi.

Songea. Mfanyabiashara wa usafirishaji mkoani Ruvuma, Jaribun Jaribun ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuacha kujisifia kukusanya Sh12 bilioni kwa mwaka mkoani Ruvuma akidai wanaumizwa kwa kuwa mkoa huo hauna viwanda.

Amesema wafanyabiashara wamechoshwa na tabia ya kupandishiwa makadirio ya mapato kila mwaka na wameshatoa malalamiko kwenye vikao mbalimbali hiyo bado hawasikilizwi.

Jaribun ametoa madai hayo mbele ya Naibu Kamishna wa TRA, Charles Kichele mjini Songea aliyekuja kuzungumza na wafanyabiashara ili kujua changamoto zinazowakabili.

“Hali za wafanyabiashara mkoani Ruvuma ni mbaya, tunaendelea kudhoofu hakuna vyanzo vya mapato, hakuna viwanda biashara zimekuwa ngumu. Wengi wameacha kutokana na kodi nyingi ambazo ni kero kwetu, “ amesema na kuongeza kuwa:

“Tunaomba Serikali itusikilize na kuondoa kodi zisizo na maana zikiwamo stika,  tunaonewa, tunaipenda nchi yetu na ndiyo maana tunalipa kodi lakini tunaumizana.”

Mfanyabiashara mwingine, Halima Kayombo ameitaka Serikali kutambua umuhimu wa wafanyabiashara na mchango wao kwa kuzifanyia kazi kero zao kwa vitendo.

Baada ya wafanyabiashara wa mkoa huo kutoa vilio vyao ikiwamo kudai kukadiriwa mapato makubwa na kurundikiwa kodi, Kichele ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko hayo.

Kichele amesema amechukua mapendekezo ya wafanyabiashara na yatafanyiwa kazi kwa kuwa malalamiko mengi yanahusu sheria hivyo hawezi kuyatolea uamuzi papo hapo.

“Muda siyo mrefu mtapata majibu ili kuondoa kero zinazowakabili. Najua kuna baadhi ya sheria kweli zinahitaji kubadilishwa lakini binafsi siwezi hadi Bunge lizibadilishe,” amesema na kuongeza kwamba:

“Nawapongeza wafanyabiashara kwa kuonyesha  mmeridhia kulipa kodi, kuna baadhi ya maeneo hali ni tofauti. Ninyi mmekuwa waungwana na wazalendo.”