Mfuko wa uhalifu waipa polisi vitendea kazi vya Sh18 milioni

Muktasari:

Zimo pikipiki na mashine mbalimbali za karakana

Wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga kupitia mfuko wao wa kukabiliana na uhalifu, jana walilikabidhi Jeshi la Polisi pikipiki na vitendea kazi vingine vyenye thamani ya Sh18 milioni.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa jeshi hilo na mwenyekiti wa mfuko huo, Abdi Awadh kwa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe.

Pamoja na pikipiki nne aina ya Sunlg zenye thamani ya Sh8 milioni mfuko huo ulioasisiwa mwaka 2007 na IGP Simon Sirro alipokuwa kamanda wa polisi mkoani hapa, pia ulikabidhi mashine ya kuwekea upepo na ya kuungia vyuma kwa ajili ya matumizi ya karakana ya jeshi hilo iliyopo jijini hapa vyote vikiwa na thamani ya Sh10 milioni.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Awadh alimweleza kamanda Bukombe kuwa mchango huo unatokana na ushirikiano baina yao na jeshi hilo katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu mkoani Tanga.

Katibu wa mfuko huo, Charles Hozza alisema wafanyabiashara hao walianza utaratibu wa kulipatia jeshi hilo vitendea kazi tangu Mei 23, 2007 chini ya Sirro lengo likiwa ni kushiriki katika suala zima la ulinzi shirikishi.

Alisema tangu kuanzishwa kwa mfuko huo, mambo mbalimbali yamefanyika kurahisisha utendaji wa polisi kiulinzi na kwamba ulishakabidhi pikipiki saba, vituo vidogo vitano vya polisi, ununuzi wa redio za upepo 15, king’amuzi mwendo na ujenzi wa gereji ya magari ya polisi na vifaa vyake.

Mambo mengine yaliyofanywa na mfuko huo kwa jeshi hilo ni kutoa mafunzo ya kompyuta kwa wakuu wa wilaya na vituo (OCD) 14, ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi kilichopo Pongwe sambamba na ulipaji wa fedha kwa askari wa jeshi la akiba (mgambo) wanaotoa huduma kwenye vituo vya polisi. Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walipongeza hatua hiyo ya wafanyabiashara kuwa karibu na jeshi hilo.

“Kulisaidia jeshi letu ni mpango mzuri unaostahili kuungwa mkono na kila mkazi wa Tanga, nadhani pia ni vizuri hata wananchi wa kawaida tukawaunga mkono wenzetu wanaounda mfuko huo,” alisema Wiwi Emmanuel.

Malamusha Kilonde alitaka uanzishwe mpango wa kila mwananchi kuchangia alichonacho kwa ajili ya jeshi ili liweze kujitosheleza kwa vifaa na magari.

Baada ya kupokea vitendea kazi hivyo, Kamanda Bukombe aliwaahidi wafanyabiashara hao na wananchi kwa ujumla kuwa msaada huo utatumika kwa manufaa ya jamii ya Tanga ili kujenga imani kwa wadau hao na wengine kuona umuhimu wa kuchangia suala la ulinzi.