Mfumuko wa bei ulilingana na wa mwaka 2004

Muktasari:

  • Kuanzia Novemba mwaka jana mpaka Mei, mfumuko wa bei ulishuka kutoka asilimia 4.4 mpaka 3.6 ambao ni wa chini zaidi kushuhudiwa kwa zaidi ya muongo mmoja. Mara ya mwisho kiwango hicho cha chini kilikuwapo Mei 2004 na hakikushuhudiwa tena kwa kipindi chote cha Serikali ya awamu ya nne.

Dar es Salaam. Wakati ikitarajia kuanza kutekeleza bajeti mpya kuanzia Julai Mosi, Serikali imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei mwaka huu wa fedha.

Kuanzia Novemba mwaka jana mpaka Mei, mfumuko wa bei ulishuka kutoka asilimia 4.4 mpaka 3.6 ambao ni wa chini zaidi kushuhudiwa kwa zaidi ya muongo mmoja. Mara ya mwisho kiwango hicho cha chini kilikuwapo Mei 2004 na hakikushuhudiwa tena kwa kipindi chote cha Serikali ya awamu ya nne.

Kupungua kwa mfumuko huo kwa mwaka ulioishia Mei kumetokana na kushuka kwa bei ya vyakula na vinywaji visivyo na kilevi kwa asilimia 2.6, usafirishaji asilimia 1.9 na huduma za mawasiliano asilimia 0.1.

Kwa miezi 10 ya mwanzo ya mwaka wa fedha 2017/18, Serikali imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kuwa wa tarakimu moja jambo linalopongezwa na wachumi.

Kati ya Juni 2017 mpaka Mei, mfumuko huo ulikuwa wastani wa asilimia 4.4 ukiwa chini ya makisio ya Serikali ya kati ya asilimia 5.0 mpaka 8.0.

Alipokuwa akiwasilisha bajeti ya mwaka 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kwa mwaka mzima 2017, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 5.3 ambao ulipungua mpaka asilimia 3.8 Aprili.

“Kupungua huko kulitokana na ongezeko la uzalishaji wa chakula, uimara wa Shilingi dhidi ya sarafu za nje, kuimarika kwa uzalishaji wa umeme, usimamizi wa sera za fedha na udhibiti wa deni la Taifa,” alisema Dk Mpango.

Kumbukumbu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kutopanda kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na mambo matatu ambao ni bei ya vyakula na vinywaji baridi vyenye asilimia 38.5 ya mahitaji yote, usafirishaji wenye asilimia 12.5 na makazi, maji, umeme na gesi kwa asilimia 11.6. Maeneo hayo yote yalikuwa na tarakimu moja.

Kwa mwaka mzima wa fedha, mfumuko mkubwa zaidi ulishuhudiwa Septemba 2017 ulipofika asilimia 5.3 ukichangiwa na kupanda kwa bei za vyakula na vinywaji baridi iliyoongezeka mpaka asilimia 9.3.

Mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi anasema mfumuko mdogo wa bei ni mzuri kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa unahamasisha uwekezaji na matumizi ya huduma na bidhaa kwa vile bei hubaki chini.

“Zipo sababu nyingi zinazochangia mfumuko kuwa chini kama vile uingizaji wa bidhaa kutoka nje au usafirishaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, uimara wa sarafu na usimamizi wa sera za fedha na uchumi,” alisema.

Mchumi mwingine wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Semboja Haji alisema mfumuko mdogo wa bei unaonyesha nchi ipo kwenye hali nzuri kiuchumi hasa usimamizi wa sera zake.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo anakumbusha kuwa ipo haja ya kuhusisha mfumuko wa bei na masuala mengine ya kiuchumi ili kuona faida yake.

“Inapendeza kuwa na mfumuko mdogo lakini usitusahaulishe ukosefu wa ajira, urari wa biashara au kiasi cha uwekezaji. Kuna nakisi kwenye urari wa biashara na ajira zinazotolewa bado ni chache,” alisema.

Kushughulikia changamoto hizo, alisema miradi ya maendeleo ya Serikali inapaswa kuzingatia ubora wa maisha ya watu kwa kutoa fursa muhimu zitakazowashirikisha hivyo kukuza kipato chao.

Katika kipindi hicho, fahirisi ya bei inayopima mabadiliko kwa bidhaa zote zilizopo sokoni ilikuwa wastani wa 110.3.