Thursday, January 11, 2018

Mfungwa wa ujangili, wenzake watatu kortini

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi amayunga@mwananchipapers.co.tz

Mfungwa Khamisi Mussa (40), mkazi wa Kibiti mkoani Pwani aliyekutwa akifanya ujangili ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, pamoja na wenzake watatu wameburuzwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.

Pamoja na Mussa maarufu kwa jina la ‘Mbweha’, wengine waliofikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Serengeti ni Hamisi Mabula (51) mkazi wa Kono, Giriena Bwanana (34) mkazi wa Bwitengi na Hamisi Gamaho (37) mkazi wa Robanda Wilaya ya Serengeti.

Wakili mwandamizi wa Serikali, Valence Mayenga alidai mahakamani kuwa washtakiwa kwa pamoja waliingia ndani ya hifadhi hiyo ya Taifa bila kibali kinyume na kifungu cha hifadhi namba 21(1)(a) na (2) na 29(1) cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa sura namba 282 na marekebisho na sheria namba 11 ya 2003.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ismael Ngaile washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 2 waliingiza silaha aina ya Riffle 458 ndani ya hifadhi kinyume na kifungu cha 24(1)(b) na (2) cha Sheria ya Hifadhi ya Taifa sura namba 282 ya 2002.

Shtaka la tatu ni kukutwa na nyara kinyume na kifungu 86(1)na (2)(iii) cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ambayo inasomwa pamoja na aya 14 jedwali la kwanza sura namba 57(1) 60 (2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura namba 200/2002 iliyorejewa na sura namba 13 na 16 ya sheria namba 3 ya mwaka 2016.

Katika shtaka la nne na tano kwenye shauri hilo namba 3/2018, washtakiwa wanadaiwa kuua tembo wawili na kukutwa na meno manne ya tembo yenye uzito wa kilo 72.4 yakiwa na thamani ya Sh64.8 milioni.

Wakili Mayenga alitaja shtaka la sita kuwa ni kumiliki bunduki na risasi kinyume na Sheria ya Kumiliki Silaha kifungu cha 4(1) na (2) na 34(1)(2) ya sura ya 223 na marekebisho ya mwaka 2002.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 23 itakapotajwa tena.

Katika tukio lingine, Hamisi Mabula (51), mkazi wa Kijiji cha Kono wilayani Serengeti amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka manne ya uhujumu uchumi. Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Serengeti, Ismail Ngaile, wakili mwandamizi wa Serikali, Valence Mayenga alitaja kosa la pili kuwa ni kuingia na silaha bila kibali wakati la tatu ni kumiliki silaha, huku la nne likiwa ni kumiliki risasi.     

-->