Mgawanyo usio sawa wa walimu unachangia elimu kushuka

Muktasari:

Uchambuzi wa takwimu za uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kwa shule za msingi za umma mwaka 2016 uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa baadhi ya mikoa yenye idadi ndogo ya wanafunzi, ina walimu wengi zaidi kuliko ile yenye idadi kubwa ya watoto hao, jambo linalovunja usawa katika upatikanaji wa elimu bora.

Licha ya jitihada za Serikali kuongeza walimu wa shule za msingi katika miaka ya karibuni, maelfu ya wanafunzi vijijini huenda wakaendelea kusubiri kwa muda mrefu kufundishwa vipindi vyote, kutokana na kuwapo kwa mgawanyo usio sawa wa watumishi hao nchini.

Uchambuzi wa takwimu za uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kwa shule za msingi za umma mwaka 2016 uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa baadhi ya mikoa yenye idadi ndogo ya wanafunzi, ina walimu wengi zaidi kuliko ile yenye idadi kubwa ya watoto hao, jambo linalovunja usawa katika upatikanaji wa elimu bora.

Mikoa inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya walimu licha ya kuwa wanafunzi wachache kuliko mingine ni Kilimanjaro, Arusha na Dar es Salaam wakati mikoa ya Kigoma, Mara, Rukwa na Mwanza ikiwa na wanafunzi wengi ikilinganishwa na mitatu ya juu yenye watumishi wengi.

Takwimu hizo za hadi Machi mwaka jana kutoka kituo cha takwimu huru cha Serikali (opendata)www.opendata.go.tz , zinaonyesha kuwa mgawanyo wa walimu usio sawia unaendelea ndani ya mikoa, wilaya hadi katika ngazi ya shule zilizopo ndani ya kata moja hata kwenye mikoa ile yenye uwiano mzuri wa mwalimu na wanafunzi kama Kilimanjaro.

Waandishi wa Mwananchi walitembelea katika baadhi ya shule zilizopo mikoa ya Tabora, Kigoma, Morogoro na Dar es Salaam na kubaini kuwa shule zilizobainishwa kwenye takwimu kuwa zina walimu wengi zinafanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya darasa la saba kuliko zile zenye uhaba jambo linalotishia mustakabali wa elimu nchini.

Katika uchambuzi huo, imebainika kuwa hata majiji ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Tanga na Mwanza ambayo wengi hupendelea kwenda uwiano kati ya walimu na wanafunzi unatofautiana.

Hadi Machi mwaka jana, Dar es Salaam iliyokuwa na wanafunzi 485,389 ilikuwa na walimu 12,813 takribani idadi sawa na wale waliopo Mwanza iliyokuwa na wanafunzi 627, 695.

Hii ina maana kuwa Mwanza licha ya kuwa na wanafunzi 142,306 zaidi ya Dar es Salaam bado ilikuwa na walimu 12,833 pekee na kufanya wastani wa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kuwa juu ya kiwango kinachotakiwa na Serikali.

Wizara ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaeleza kuwa uwiano sahihi kwa shule za msingi ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 (1:40), lakini Mwanza mwalimu mmoja anafundisha wastani wa watoto 54 wakati Dar es Salaam anafundisha watoto 38.

Uwiano huu usio linganifu wa walimu upo kila mahali. Mkoa wa Simiyu uliokuwa na wanafunzi 333,601 ulikuwa na walimu 7,093 tu pungufu ya wale waliopo Arusha uliokuwa na wanafunzi 262,117. Arusha ilikuwa na walimu 7,605. Hii ina maana kwamba Arusha ina walimu 500 zaidi ya wale waliopo Simiyu licha ya kuwa na wanafunzi 71,484 zaidi.

Ugawaji huo wa walimu usio sawa umefanya Simiyu iwe na uhaba mkubwa wa walimu na kufanya uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kuwa 1:52 dhidi ya Arusha yenye uwiano wa mzuri wa 1:37.

Uwiano kati ya mwalimu na wanafunzi umekuwa ni moja ya kigezo kikubwa katika kutathmini kiwango cha ufaulu wa shule husika ambapo kwa miaka mingi, shule zenye uwiano mzuri zimekuwa na kiwango kizuri cha ufaulu kuliko zenye uwiano mbaya.

Licha ya uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi unaopendekezwa kuwa ni 1:40, takribani nusu ya shule za msingi zilizopo mkoani Ruvuma zipo juu wa wastani huo wakati Kilimanjaro ikiwa na shule takribani robo tatu zenye uwiano mzuri.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, Kilimanjaro wenye wanafunzi 253,263 ulikuwa na walimu 8,297 ambao ni sawa na watumishi 1,962 zaidi ya waliopo Ruvuma.

Ruvuma uliokuwa na wanafunzi 271,201 wengi kidogo zaidi za Kilimanjaro huku idadi ya walimu ikiwa ni 6, 341 tu kufanya mwalimu mmoja afundishe wastani wa wanafunzi 47.

Pamoja na kwamba uwepo wa walimu wa kutosha si kigezo pekee cha utoaji wa elimu bora, lakini mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha inayoongoza kuwa na uwiano mzuri wa mwalimu kwa wanafunzi, imekuwa ikipata kiwango kizuri cha ufaulu katika mitihani ya Taifa ya kumaliza elimu za msingi.

Mikoa hiyo imekuwa ikiingia kwenye 10 bora inayofanya vizuri zaidi katika mitihani ya Taifa ya darasa la saba kwa takriban miaka mitatu mfululizo wakati mikoa ya Kigoma, Dodoma na Tabora yenye idadi ndogo ya walimu ikiwa na ufaulu wa wastani.

Kwa miaka mingi, Tanzania imekumbwa na uhaba wa walimu katika shule za umma hasa wa masomo ya hesabu na sayansi licha ya Serikali kujitahidi kuajiri takribani kila mwaka.

Hadi Desemba 2016, takwimu za Tamisemi zinaonyesha kuwa kulikuwa na upungufu wa walimu takribani 47,151 katika shule za msingi za umma.

Nini kinawakimbiza walimu?

Mbali na uchambuzi wa kitakwimu, waandishi wetu walibaini katika uchunguzi wao kuwa pamoja na upangaji usio sawa wa watumishi wa umma, zipo sababu nyingine zinazosababisha walimu wengi kurundikana mijini ikiwamo mazingira magumu ya kufundishia yaliyopo katika shule za vijijini.

Mazingira hayo, yanayochagizwa zaidi na miundombinu mibovu, ukosefu wa huduma za jamii na uhaba wa nyumba za walimu katika shule zilizopo vijijini, yamesababisha shule hizo kubakia na walimu wachache wanaovumilia changamoto hizo.

Katika baadhi ya maeneo, walimu hujenga nyumba zao za kuishi ikiwemo za udongo kutokana na shule zao kutokuwa na nyumba za watumishi au zinazofaa kupangishwa.

Kwa mfano, katika Shule Msingi Chohero iliyopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro walimu hulazimika kutembea kwa miguu katika milima ya Uluguru takriban kilomita 20 kwa kuwa hakuna barabara ya magari.

Shule hiyo yenye walimu wawili ambao hadi Disemba, 2016 walikuwa wakifundisha wanafunzi 510. Hayo ni kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu, Bernard Pius.

Katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana, ilikua ni miongoni mwa shule 10 zilizoshika mkia nchini baada ya kufaulisha wanafunzi sita tu kati ya 49 waliofanya mtihani huo. Chohero ina madarasa mawili yanayofaa kutumika na nyumba mbili za walimu.

Ofisa Elimu Mkoa wa Kigoma, Omari Mkombole anasema kuwa tofauti ya idadi ya walimu kutoka mkoa mmoja hadi mwingine, husababishwa na baadhi ya watumishi hao kushindwa kuhimili maisha ya vijijini na hivyo kuomba kubadilishwa vituo ama kuacha kazi na kuhamia shule binafsi.

“Lakini kama Serikali itaboresha motisha kwa walimu wanaopangiwa vijijini na maeneo ya pembezoni, walimu wengi wangeweza kubaki huko.

“Kwa mfano, sisi Kigoma tumeshaanza michakato ya kuangalia namna ya kuongeza viwango vya motisha na maelekezo tayari yameshapelewa kwa viongozi wa wilaya kuhakikisha hili linafanikiwa ili kuziokoa shule zilizopo maeneo yenye changamoto,” anasema Mkombole.

Serikali yafafanua

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu wa Tamisemi, Juma Kaponda anakiri kuwapo maeneo yenye walimu wengi kuliko mengine akibainisha kuwa hali hiyo inachangiwa na sababu za kijamii, kiafya na kiutendaji.

Anasema ugawaji wa walimu huangalia kwanza aina ya masomo yanayotolewa katika shule husika, lakini pia idadi ya mikondo ya madarasa iliyopo katika shule husika.

Kwa mfano, anasema kuna shule zina darasa la kwanza hadi la saba lakini zikiwa na mkondo mmoja mmoja wakati nyingine zina mkondo zaidi ya mmoja, hivyo idadi ya walimu katika shule hizo lazima itofautiane, huku zile zenye mikondo mingi zikipata walimu wengi zaidi.

Anataja sababu nyingine zinazochangia hali hiyo kuwa ni masuala ya kifamilia hususan kwa walimu wa kike ambao hulazimika kuvihama vituo vya kazi walivyopangiwa awali ili kuwafuata waume zao.

“Lakini pia, mwalimu anaweza kuwa mgonjwa anayehitaji huduma maalumu kwa mujibu wa ripoti za madaktari, hivyo badala ya kumwacha katika mkoa fulani bila matibabu, tunamhamisha na kumpeleka mahali ambapo atakua anapata matibabu huku akiendelea kufundisha,” anasema Kaponda.

Hata hivyo, anabainisha kwamba walimu wanaozidi katika maeneo fulani ni upotevu wa nguvu kazi na wanatakiwa wasambazwe upya katika shule zenye uhaba.

“Tumeshatoa maelekezo kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanapeleka idadi ya walimu inayotakiwa katika shule zote zenye upungufu wa walimu. Pia, Serikali mwaka huu ina mpango wa kuajiri walimu 10,169 wa masomo ya hesabu na sayansi kwa shule za sekondari na 40,000 kwa shule za msingi kuziba mapengo hayo,” anaongeza.

Wasemavyo wadau

Baadhi ya wataalamu wa elimu wameeleza kuwa uwiano usio sawa, unatokana na kukosekana kwa sera ya motisha kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira duni.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Luka Mkonongwa, anasema hali mbaya ya mazingira ya kazi katika maeneo mengi ya vijijini huchangia baadhi ya walimu kudanganya kuwa wanasumbuliwa na maradhi ili wahamishiwe katika shule za mjini ili kupata matibabu zaidi.

“Hii ni changamoto kubwa sana ambayo inaathiri ubora wa elimu, ni ngumu sana kwa shule isiyokua na walimu wa kutosha kuwa na kiwango kizuri cha ufaulu lakini pia ni ngumu kukataza uhamisho kutokana na sababu za afya na ndoa.

“Hivyo ili kutatua suala hili, tunapaswa kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii katika maeneo yote nchini, lakini pia kutoa motisha kwa walimu wanaoishi vijijini,” anasema.