Mghwira aibuka ghafla kiwandani, alizwa maagizo kutotekelezwa

Muktasari:

Hayo yalijitokeza jana baada ya Mghwira kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda hicho ambacho ni moja kati ya viwanda vilivyosimamisha uzalishaji baada ya kubinafsishwa mwishoni mwa miaka ya 1990.

Moshi. Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira, ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL) katika kufufua Kiwanda cha Magunia (TBC) mjini hapa.

Hayo yalijitokeza jana baada ya Mghwira kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda hicho ambacho ni moja kati ya viwanda vilivyosimamisha uzalishaji baada ya kubinafsishwa mwishoni mwa miaka ya 1990.

Tayari Rais John Magufuli amemwagiza waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuwanyang’anya viwanda wawekezaji walioshindwa kuviendeleza baada ya kubinafsishwa.

Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, mkuu wa mkoa alisema Septemba walitembelea kiwanda hicho na kutoa maagizo ya kuanza uzalishaji.

Katika ziara hiyo, uongozi wa MeTL ulieleza changamoto inayofanya washindwe kukifufua kuwa ni kuziba kwa mitaro ya maji na kusababisha maji na matope kujaa kiwandani mvua zinaponyesha.

Mghwira alisema kutokana na changamoto hiyo, aliagiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuzibua mitaro iliyo chini yao na uongozi wa kiwanda nao uzibue iliyopo ndani.

“Maandalizi ya usafi tulikuwa tumekubaliana ni Septemba hadi Oktoba. Maandalizi ya kazi kuanza yalikuwa ni Novemba na Desemba ili Januari angalau tuone uzalishaji umeanza,” alisema mkuu wa mkoa.

Msimamizi wa kiwanda hicho aliyekutwa na mkuu wa mkoa, Sadick Haji alisema atafikisha ujumbe na maagizo hayo kwa mmiliki wa kiwanda, ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Danford Kamenya alisema wao walipewa kazi ya kusafisha mitaro mikubwa inayoelekea kiwandani na wameifanya na kuikamilisha.

Katika ziara hiyo Mghwira alikutana na Diwani wa Njoro (Chadema), Jomba Koyi mahali kilipo kiwanda hicho na kumlaumu kuwa hawajatimiza wajibu wao wa kuwabana wawekezaji.

Hata hivyo, diwani huyo alijitetea akisema kwamba ilikuwa vigumu kuingilia viwanda hivyo wakati vikiwa chini ya wamiliki binafsi, lakini wanazo kumbukumbu katika halmashauri namna walivyovipigia kelele virudishwe Serikalini.