Mgogoro CCM Arusha kuwaathiri wananchi

Muktasari:

CCM inajipanga kumvua uanachama Sabaya ambaye pia alisimamishwa uenyekiwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani hapa kwa tuhuma za kukiuka maadili.

Arusha. Wakazi wa Kata ya Sambasha wilayani Arumeru wanaweza kukosa mwakilishi kwenye baraza la madiwani iwapo mpango wa CCM Mkoa wa Arusha wa kumvua uanachama diwani wao, Lengai ole Sabaya utatekelezwa.

CCM inajipanga kumvua uanachama Sabaya ambaye pia alisimamishwa uenyekiwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani hapa kwa tuhuma za kukiuka maadili.

Hivi karibuni Sabaya alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha na kusomewa mashtaka ya kujifanya ofisa usalama wa Taifa na kughushi kitambulisho cha ofisi hiyo. Yuko nje kwa dhamana.

Akizungumza kwa simu kuhusu mpango wa kuvuliwa uanachama, Sabaya alisema hakuna mwenye mamlaka kisheria ya kufanya hivyo na iwapo hilo litafanyika anasubiri uamuzi huo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya CCM Kata ya Sambasha ilikutana kumjadili Sabaya na kuwasilisha mapendekezo kwa uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya kwa hatua zaidi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Leimon Mollel ambaye hakuzungumzia kwa undani uamuzi wa kikao hicho, alisema kilihudhuriwa na wajumbe 16 kati ya 24 na wanne walitoa udhuru.

Katibu wa CCM wilayani Arumeru, Godfrey Sabuni alisema walipokea mapendekezo hayo juzi na kikao kitaandaliwa kuyajadili kabla ya kuwasilishwa kwa uongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa.

Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa wa Arusha, Omary Bilal alisema uongozi huo umetoa muda hadi Oktoba 31, ngazi ya kata na wilaya kukamilisha mapendekezo ndipo utatoa uamuzi.