Majaliwa amaliza mgogoro wa Loliondo

Muktasari:

Wizara ya Maliasili na Utalii imeagizwa iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalumu au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo uliodumu kwa takriban miaka 26.

Hatima hiyo ilifikiwa jana Jumatano Desemba 6,2017 kwenye kikao kilichoitishwa na waziri mkuu ofisini kwake Mlimwa mjini Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya kamati ya uchunguzi.

Waziri mkuu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake leo Alhamisi Desemba 7,2017 amesema Serikali imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalumu kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.

“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalamu ilipendekeza kuwa utumike mfumo utakaounda chombo maalumu, kwa kuwa una masilahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,” amesema.

Waziri mkuu ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalumu au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo.

“Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia masilahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya ardhi,” ameagiza waziri mkuu.

Pia, ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalumu utakaowasilishwa serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Amesema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili waipitie kwanza.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/2019.

Pia, amewaagiza mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya pori tengefu la Loliondo wafanye ziara kutembelea eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo.