Mgogoro fedha za ujenzi makao makuu ya wilaya wamtibua JPM

Dar es Salaam/Tanga. Rais John Magufuli ameagiza Sh1.5 trilioni zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Wilaya ya Bumbuli zirejeshwe Hazina ili zipangiwe matumizi kutokana na viongozi wake kulumbana kuhusu eneo linalostahili kujengwa.

Rais alisema hayo jana wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ikulu jana.

“Jana niliandikiwa barua na waziri wa Tamisemi, kuhusu wilaya ya Bumbuli, wanabishana kwa fedha zilizopelekwa kule kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kujenga makao makuu ya wilaya,” alisema.

“Viongozi wanabishana ujenzi haufanyiki, Mkuu wa Mkoa akataka kuzichukua ili zijenge hospitali bado amepingwa, jana nikatoa maelekezo fedha zirudishwe Hazina.”

Alisema tatizo hilo limekuwa likichagizwa na wanasiasa katika eneo husika hatua inayosababisha kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

Mzozo wenyewe

Akizungumzia mzozo wa ujenzi huo wa makao makuu ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Sigareti alisema kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa wa Tanga (RCC) cha Machi 9 kiliridhia makao hayo yajengwe eneo la Kwehangala ikiridhia ombi la Bumbuli lakini hoja hiyo ilipowasilishwa kikao cha kamati ya ushauri ya maendeleo Wilaya ya Lushoto kiliamua yajengwe mahala ambako hivi sasa kuna majengo ya watumishi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli, Amir Shehoza alisema hajui kwa nini mgogoro huo umeibuliwa tena wakati kikao cha RCC Tanga kilichohudhuriwa pia na wabunge, kilibariki uamuzi wa kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Bumbuli kwamba makao makuu yajengwe Kwehangala.

“Taratibu zote zilifuatwa tulifanya maamuzi kwenye Full Council (Baraza Kuu) tukiwa madiwani 18, wote tulikubali makao makuu yajengwe Kwehangala kwa sababu tayari Tamisemi ilishatoa Sh400 milioni kwa ajili ya ununuzi wa eneo, sasa huyu anayepinga (bila kumtaja jina) sijui ana nguvu gani,” alisema Shehoza.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema anakubaliana na uamuzi wa Rais Magufuli kwamba fedha hizo zirejeshwe hazina kama hakutakuwa na maelewano kwa sababu kuna mchezo mchafu unaotaka kufanyika wa kuzihamishia kwenye matumizi mengine.

“Rais ametusaidia madiwani wa Bumbuli, nimefurahi na nakubaliana naye kwamba kama huyo anayepinga uamuzi wa madiwani na wajumbe wa RCC hataki kwa sababu ya nguvu zake serikalini basi ni bora fedha hizo zirejeshwe kwa Rais kwa sababu zitakuwa mahala salama,” alisema Shehoza.