Mgombea Chadema azidi kuporomosha ahadi

Arusha. Mgombea udiwani wa Muriet kupitia Chadema, Simon Moses amewaahidi atakapochaguliwa ataweka makaravati kuondoa kero ya maji kutuama kila mtaa kipindi cha mvua.

Moses alisema hayo juzi katika kampeni zilizofanyika kwenye Mtaa wa Bondeni, ambao una mitaro ambayo haina makaravati.

Alisema atawaondolea wananchi kero hiyo hasa wanafunzi wanaoshindwa kupita wanapokwenda na kutoka shuleni.

“Naelewa kuwa hiyo ni changamoto kubwa ambayo mnakabiliana nayo katika kata hi hasa kipindi cha mvua maji yanakuwa mengi. Nawaahidi nitaanza nalo hili nanyi wenyewe hamtajuta kunichagua,” alisema Moses.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi kuhusu kutakiwa kulipia Sh200,000 ili kuendeleza maeneo waliyonunua, Moses alisema huo ni uvunjaji wa sheria unaofanywa na mwenyekiti wa mtaa na kamwe hatalifumbia macho suala hilo.

Mgombea huyo alisema hakuna sheria yoyote inayomtaka mnunuzi kulipa fedha kwa ajili ya kuendeleza eneo alilonunua, hivyo aliwataka kutolipa chochote na kuendeleza maeneo yao bila shuruti.

Aliwaahidi atakapochaguliwa suala hilo atalivalia njuga kwa kuhakikisha wanashughulika na wote wanaokiuka sheria na kuwanyanyasa wananchi.

Pia, Moses aliwaahidi wananchi hao kushughulikia kero ya maji ambalo ni tatizo kubwa katika mtaa huo na kata kwa jumla.

“Naombeni mnichague muone namna ambavyo nitawafanyia mambo makubwa ndani ya kata hii, maana naelewa pakuanzia na kumalizia ndiyo maana nimeamua kugombea ili niwasaidie wananchi kuondokana na changamoto zinazowakabili,” alisema Moses.